Chama cha Kiorthodox kujiondoa kwenye serikali ya Netanyahu
15 Julai 2025Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti Jumanne kuwa chama hicho chenye imani kali za Kiyahudi kinachoiwakilisha jumuiya ya Haredi, hakijaridhishwa na muswada wa sheria uliowasilishwa siku ya Jumatatu wa kudhibiti shughuli za kijeshi kwa waumini wa madhehebu ya Kiorthodox.
Wabunge wa chama hicho, akiwemo naibu waziri wa usafiri na waziri wa masuala ya Jerusalem wanatarajiwa kujiuzulu serikalini.
Chama hicho kina viti saba katika Bunge la Israel, lenye jumla ya viti 120.
Wakati huo huo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na haki za binaadamu, imesema Jumanne kuwa pamekuwepo na ongezeko la mauaji na mashambulizi dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na walowezi na vikosi vya usalama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu katika wiki za hivi karibuni.