Chadema yamjibu Msajili kwamba haitobadilisha chochote
14 Mei 2025Makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara, John Heche ambaye yuko katika ziara ya kunadi ajenda ya "bila mabadiliko hakuna uchaguzi" amesema kumekuwa na mbinu chafu zinazoendelea kuratibiwa ili kuivuruga chadema inayoendelea kuandamwa na mfulilizo wa matukio.
Amesema viongozi wa chama waliotajwa kung'olewa na msajili wa vyama vya siasa akiwamo katibu mkuu wa chama John Mnyika wapo kwa kwenye nyadhifa zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za chama.
"Msajili, huitaji kumtambua Katibu Mkuu wa chama chetu. Sisi Chadema tunamtambua Katibu Mkuu wa chama chetu", Heche aliwambia wafuasi wa Chadema.
Hapo jana, Msajili wa Vyama vya Siasa alitangaza kutengua uteuzi wa viongozi sekretariati ya CHADEMA inayoongozwa na katibu mkuu John Mnyika ambayo iliteuliwa baada ya uchaguzi wa ndani wa CHADEMA uliofanyika Januari 22 Jijini Dar es salaam.
"Hii mbinu nayo itashindwa"
Uchaguzi huo unatajwa kuzua sokomoko linaloonekana kuanza kuwagawa baadhi ya wanachama na viongozi kutokana na kambi za pande mbili, ya mwenyekiti aliyeondoka Freeman Mbowe na yule aliyeshinda Tundu Lissu
Ama waliotajwa kutotambuliwa na msajili siyo viongozi halali ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa Bara Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar Aly Ibrahim Juma, na wajumbe watano walioteuliwa kuingia kwenye Kamati Kuu ya chama.
Mnyika amesema chama hiko kimejipanga kukabiliana na tamko la msajili wa vyama vya siasa, akisisitiza suluhu ya mwwsho litapatikana mahakamani.
"Nataka kuwaambia waliotumwa : Hii mbinu nayo itashindwa. Safu yetu ya mawakili imekwisha jipanga kwa mapambano mahakamani."
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara, Amani Golugwa ambaye alikamatwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Nyerere Jumatatu usiku na kushikiliwa kituo cha polisi cha kati kwa madai huwa "anasafiri nje ya nchi mara kwa mara na kurudi nchini bila kufuata utaratibu" aliachiliwa na polisi jana usiku.
Kiongozi huyo alikuwa anakwenda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Watetezi Duniani IDU unaofanyika Brussels, Ubelgiji.
Viongozi wengine wa Chadema waliokwenda kituo kikuu cha polisi mjini Dar es Salaam kwa ajili kumwekea dhamana Golugwa lakini nao walikamatwa na kuswekwa ndani pia waliachiwa Jumanne usiku.