CHADEMA yakemea kunyimwa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu
15 Aprili 2025Matangazo
Mwanasheria mkuu wa chama hicho Rugemeleza Nshala amesema hoja ya chama hicho cha Chadema ni kwamba hatua zilizochukuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi zinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mnamo siku ya Jumapili Tume ya Uchaguzi nchini humo ilitangaza kukipiga marufuku chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba na chaguzi nyingine zitakazofanyika katika kipindi cha miaka mitano. Uamuzi huo umefikiwa baada ya CHADEMA kutotia saini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi. Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu, ambaye alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini wiki iliyopita, awali alisema kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi bila mageuzi ya uchaguzi.