CHADEMA: Vuguvugu letu ni la kutaka mageuzi sio uhaini
11 Aprili 2025Akizungumza na wanahabari Ijumaa, naibu katibu mkuu wa chama hicho CHADEMA , Amani Golugwa amewaambia wanahabari kuwa vuguvugu la hakuna mageuzi hakuna mabadiliko, halimaanishi uasi bali chama hicho kipo kinyume na mifumo mibovu ya uchaguzi.
Kadhalika Goluwa amesema Tanzania inadai mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, sheria za uchaguzi ili kuwepo kwa chaguzi za haki na wazi Tanzania.
CHADEMA yasema maana yao ya uasi ni kwenda kinyume na mifumo mibaya
Golugwa amesema maana halisi ya uasi wanayoimaanisha ni Kwenda kinyume na mifumo mibaya, na kwamba chama hicho hakijatishia maisha ya rais, bali wanataka haki na chama hicho kipo kinyume na mifumo mibovu.
Golugwa ameyasema hayo leo ikiwa ni saa chache baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kusomewa mashtaka matatu, uhaini, kusema uongo na uchochezi, kisha kupelekwa rumande, bila dhamana hadi Aprili 24 kesi yake itakaposomwa.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, Lissu alikamatwa na jeshi la polisi mkoani Ruvuma, wilayani Mbinga na kusafirishwa usiku kwa usiku hadi jijini Dar es Salaam ambako jana alisomewa mashtaka hayo matatu.
Pamoja na kuzuiwa kwa mikutano hiyo na kukamatwa kwa Lissu, kadhalika jeshi la polisi lilitumia mabomu ya machozi kuwaondoa wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya katika eneo la Mfuranyaki ambako mkutano wa Lissu ulipangwa kufanyika leo.
Chadema kumchukulia hatua msemaji wa CCM kutokana na kauli tata
Muunganiko wa Vyama vya siasa duniani (IDU) nao umetoa tamko lao wakizitaka mamlaka nchini Tanzania kumwachia huru Lissuna kumwondolea mashtaka ya uhaini.
Jana baada ya kusomewa mashtaka hayo, alipelekwa rumande na kesi yake inatarajiwa kusikilizwa Aprili 24 mwaka huu.