Chad: Succes Masra ahukumiwa Kifungo cha Miaka 20
10 Agosti 2025Hii ni baada ya kumpata na hatia ya kutoa matamshi ya chuki, chuki dhidi ya wageni, na kuchochea mauaji ya halaiki.
Masra, ambaye ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Rais Mahamat IdrissDeby Itno, amehukumiwa kwa kuchochea ghasia kati ya jamii zilizosababisha vifo vya watu 42 mnamo Mei 14. Mahakama hiyo ya kwenye mji mkuu N´Djamena pia ilimtoza faini ya faranga bilioni 1 sawa na euro milioni 1.5.
Kwa mujibu wa mahakama, wengi wa waliouawa katika mauaji hayo walikuwa wanawake na watoto katika mji wa Mandakao, kusini-magharibi mwa Chad. Awali mwendesha mashtaka wa serikali alipendekeza kifungo cha miaka 25.
Hata hivyo wakili mkuu wa upande wa utetezi Francis Kadjilembaye amedai mteja wake amehukumiwa "kwa msingi wa jalada lisilo na ushahidi, kwa dhana tu na bila ushahidi wowote" akiitaja hukumu hiyo kama "matumizi ya mahakama kama silaha ya kisiasa."