Chad na Sudan Kusini zamkosoa Naibu Mkuu wa jeshi la Sudan
25 Machi 2025Wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini imetoa taarifa ikielezea wasiwasi wake mkubwa na kuikosoa vikali kauli ya Luteni Jenerali Atta iliyoiita ya kizembe.
Imekosoa hasa tamko la Jenerali huyo, kwamba serikali ya Sudan pamoja na jeshi lake ziko tayari kuchukua hatua dhidi ya wale iliyowaita wasaliti nchini Sudan Kusini.Mashambulizi ya RSF yauwa watu watatu Omdurman baada ya kupigwa na jeshi
Soma pia:
Wizara hiyo ya mambo ya kigeni imesema matamshi hayo sio tu ya kizembe na kichokozi bali pia ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni za ujirani mwema na sheria za kimataifa.
Kulingana na tovuti ya habari ya Tribune News iliyoko Paris Ufaransa, Sudan Kusini ilimuita balozi wa Sudan kutaka ufafanuzi zaidi kuhusu tamko la luteni jenerali Atta.
Wizara ya mambo ya nje ya Chad pia ilikosoa tamko la Atta pamoja na vitisho vya kuishambulia kijeshi kwa madai ya kuwaunga mkono wanamgambo wa RSF.
Chad ilikosoa vikali pia kitisho cha Atta, alichokitoa cha kuvilenga viwanja vyake vya ndege kama hatua ya kutangaza vita iliyotolewa Machi 23. Wizara hiyo imesisitiza kwamba Chad ina haki ya kujilinda kwa nguvu zote iwapo itashambuliwa.
Atta alisema nini hasa kilichofanya matamshi yake yakosolewe?
Jenerali huyo wa Susan Luteni generali Yasir al-Atta, aliituhumu Chad kwa kuikubalia Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, kupeleka silaha kwa RSF kupitia viwanja vyake vya ndege mjini N'Djamena na Amdjarass akisisitiza kuwa viwanja hivyo, ndivyo vitakavyolengwa.
Umoja wa falme za kiarabu, umekanusha madai hayo ingawa wataalamu wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa Marekani wamesema madai hayo ni ya msingi.
Kwa sasa, Khartoum imepeleka malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ikiishutumu UAE kuwa mshirika katika mauaji ya kimbari dhidi ya kabila la Masalit mjini Darfur.
Kikosi cha wanamgambo wa RSF kinachoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo aliyekuwa makamu wa kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan ni adui mkubwa wa serikali hiyo ambayo imekuwa vitani na wanamgambo hao kwa takriban miaka miwili.
Vita hivyo vilivyoanza mwezi Aprili 2023 vimesababisha mamilioni ya watu kukosa makaazi na pia kutia doa mahusiano ya Sudan na mataifa jirani.
Licha ya juhudi za Chad na Sudan Kusini kutaka maelewano bado Sudan inaendelea kuwashutumu kuwaunga mkono RSF.