Bush aunda halmashauri ya kukagua makosa kuhusu vita vya Iraq
7 Februari 2004Matangazo
WASHINGTON: Kufuatana na kuzidi malalamiko kuhusu vita vya Iraq, Rais George W. Bush wa Marekani ameunda halmashauri maalumu isiyopendelea ili kuchunguza makosa yaliyofanywa na mashirika ya upelelezi ya Kimarekani kabla ya kuanza vita vya Iraq. Kama Wenye Kiti wa Halmashauri hiyo, Rais Bush amewateua Seneta wa Chama cha Kidemokrasi Chuck Robb na Hakimu Lawrence Silverman. Halmashauri hiyo imepewa muda mpaka Machi 2005 kufanya taftishi zake, ikiwa na maana kuwa matokeo yake yatatolewa muda mrefu baada ya kumalizika uchaguzi wa Rais wa Marekani hapo Novemba mwaka huu. Halmashauri hiyo imekabidhiwa jukumu la kuchunguza kwa nini hazikuthibitika hadi sasa zile ripoti za mashirika ya kijasusi ya Marekani kuwa Irak ikidhibiti silaha za kuangamiza. Marekani na Uingereza zilitumia hoja hiyo ya silaha za kuangamiza kuhalalisha vita vyao dhidi ya Iraq.