Burundi yatoa orodha ya wahanga wa migogoro mbalimbali
29 Aprili 2025Siku ya Jumatatu, tume hiyo ilitangaza orodha za watu zaidi ya elfu 57, waliokufa ama kupotea katika mikoa ya Gitega na Mwaro katikati mwa Burundi kuanzia mwaka 1985 hadi 2008 ulipomalizika uasi nchini humo. Baadhi ya raia wanakaribisha zoezi hilo, wengine wanaomba waliokufa wafukuliwe na wafanyiwe mazishi ya heshima, huku wengine wakiomba serikali ilipe fidia.
Zoezi limetekelezwa baada ya sensa ya kitaifa
Zoezi hilo limekuwa likitekelezwa baada ya kufanyika sensa katika mikoa mbali mbali ya nchi, na hususani ile inayopakana na nchi za jirani Tanzania, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, kunakoaminika kuuawa watu wengi wakati wa vita vilivyoisibu Burundi.
HRW: Baraza la Usalama liendelee kuichunguza Burundi
Katika mikoa ya Mwaro na Gitega, tume hiyo ya ukweli na maridhiano ilibandika orodha ya watu wanaokadiriwa kufika elfu 57, waliouwawa ama kupotea kuanzia mwaka 1985 hadi 2008, ulipomalizika uasi nchini humo.
Idadi kubwa ya wahanga wa mauaji hayo ilichapishwa katika tarafa za Nyabihanga, Kayokwe na Gisozi mkoani Mwaro.
Katika tarafa ya Nyabihanga mkoani Mwaro katikati mwa Burundi alikozaliwa hayati Rais Melchior Ndadaye, waliopoteza ndugu zao walikuwa na misimamo inayotofautiana.
Human Rights Watch na hali nchini Burundi
Mmoja wa raia anasema baada ya orodha hiyo kuwekwa hadharani, suala muhimu ni maiti kufukuliwa na kufanyiwa mazishi ya heshima.
Raia mwengine Hakizimana Oscar, anasema baba yake na ndugu zake waliuwawa 1993 na kwa upande wake akatoa wito wa fidia kutoka kwa serikali.
Mkuu wa tume hiyo ya kutafuta ukweli na maridhiano, Pierre Claver Ndayicariye, amesema zoezi hilo litasaidia raia kujuwa ukweli wa kile kilichotokea, hali itakayowezesha kukarabatiwa kwa Burundimpya na kuepusha kutojirudia kwa hali hizo.
Hata hivyo, raia wengine wamekosoa kufanyika kwa zoezi hilo na kusema linafufua uchungu walio nao.
Uwepo wa tume hiyo ya ukweli na maridhiano, kunatokana na mkataba wa Arusha uliosainiwa mwaka 2000 na kupelekea kumalizika vita vilivyoisibu Burundi tangu 1993.