Burundi yaonya kuhusu kutokea kwa vita vipana vya kikanda
1 Februari 2025Rais Ndayishimiye wa Burundi ameitoa kauli hiyo Ijumaa jioni alipokuwa akizungumza na wanadiplomasia mjini Bujumbura huku video kadhaa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Ndayishimiye alisema: "Ikiwa Mashariki mwa Kongo haitokuwa na amani, eneo hilo haliwezi kuwa na amani. Ikiwa itaendelea hivi, kuna hatari ya vita kuenea katika ukanda mzima." na kuongeza kuwa : "Kama Rwanda itaendelea kutaka kuchukua maeneo zaidi na najua vita vitafika hadi Burundi, hatutokubali na vita vitaenea kote na mjiandae kwa matokeo yake."
Burundi iliwatuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuliunga mkono jeshi la Kongo. Wanajeshi wa kikosi hicho cha EAC ispokuwa wanajeshi wa Burundi walishutumiwa na DRC pamoja na wakazi wa eneo hilo kwa kushirikiana na vikosi vinavyoipinga serikali ya Kinshasa.
Kongo, Burundi zashirikiana kuwadhibiti M23
Wanajeshi wa Burundi wamevisaidia vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwadhibiti waasi wa M23 kuelekea mji wa Bukavu, huku wakifanikiwa pia kuchukua tena udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yametekwa na waasi hao.
Mashambulizi ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 yameonekana kudhibitiwa siku ya Jumamosi (01.02.2025) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya jeshi la Kongo likisaidiwa na askari wa Burundi kupata mafanikio kadhaa kwenye uwanja wa vita. Hayo yameelezwa na vyanzo kadhaa ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia na maafisa wa eneo hilo.
Soma pia: Jeshi la Kongo, washirika wa Burundi wapunguza kasi ya M23 kuelekea Bukavu
Baada ya waasi hao wa M23 kuuteka mji mkuu wa Kivu Kaskazini wa Goma, kunakopatikana migodi muhimu ya dhahabu, coltan na madini mengine, sasa walianza kuelekea jimbo la Kivu Kusini wakiulenga mji wake mkuu wa Bukavu, lakini waasi hao wameonekana kuzuiliwa tangu Ijumaa na wanajeshi wa Kongo wakisaidiwa na jeshi la Burundi.
Afisa wa eneo hilo amesema jeshi la Kongo limeimarisha uwepo wake huko Kalehe na kuchukua tena udhibiti wa vijiji kadhaa vikiwemo Mukwija vilivyokuwa vilitekwa na M23. Chanzo kingine ambacho hakikutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, kimesema mapigano yalikuwa yakiendelea sehemu mbalimbali lakini chanzo kingine cha mashirika ya kiraia kilisema hakukuwa na mapigano Jumamosi asubuhi huko Kalehe.
Wanajeshi wa Burundi wamekuwa wamekuwa wakishirikiana na vikosi vya Kongo ili kuviimarisha huko Kivu Kusini na mahali pengine kwa ombi la serikali ya Kinshasa. Wanajeshi hao wa Burundi ni miongoni mwa vikosi vinavyolenga kuizuia M23 inayoungwa mkono na Rwanda kusonga mbele kuelekea kwenye mji wa kaskazini wa Kavumu, unaopatikana kilomita 35 kaskazini mwa Bukavu kunakopatikana uwanja wa ndege na ghala la idadi kadhaa za ndege na droni za jeshi la Kongo.
Kiongozi wa mashirika ya kiraia Justin Mulindangabo, anayeishi Kavumu, amesema hali katika mji huo ilikuwa shwari siku ya Jumamosi, na wakazi ni watulivu na hawana tena hofu na wanaendelea na shughuli zao za kila siku. Hata hivyo jeshi la Kongo na lile la Burundi wamekataa kuzungumzia chochote juu ya hali inayoendelea Mashariki mwa Kongo, huku M23 wakiwa pia hawajatoa tamko lolote.
Hali ya kibinaadamu ni mbaya mno huko Goma
Wizara ya afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema siku ya Jumamosi kwamba kulikuwa na miili 773 katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika hospitali za Goma, kufuatia mashambulizi ya wiki hii yaliyofanywa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Wizara hiyo imetahadharisha kuwa vyumba vya kuhifadhia maiti vimeelemewa huku kukiwa bado kuna miili ambayo bado imetapakaa mitaani na kuongeza kuwa kuna jumla ya majeruhi 2,880 walioorodheshwa kati ya Januari 26 na Januari 30, 2025.
Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti wa Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) Jean Kaseya amesema hali katika mji mkuu wa Kivu Kaskazini wa Goma imefikia katika kiwango cha "dharura kamili ya afya ya umma", akitahadharisha kuwa mapigano yanayoendelea eneo hilo yanaweza kuchochea miripuko ya magonjwa kama Mpox, surua, kipindupindu na magonjwa mengine ambayo yanaweza kugharimu maisha ya maelfu ya watu.
(Vyanzo: AFP, Reuters, AP)