Burkina Faso yadai kutibua njama ya mapinduzi
22 Aprili 2025Akisoma tangazo la taarifa hiyo kupitia televisheni ya taifa kwenye mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, Waziri wa Ulinzi Mahamadou Sana amesema taarifa za kijasusi nchini humo zimebainisha kuwa mashambulizi hayo aliyoyaita ya kigaidi yalikuwa yamepangwa kufanyika Jumatano wiki iliyopita.
''Kitengo cha ujasusi kimeifuatilia njama ambayo, kulingana na mpango wa magaidi, ingetekelezwa Jumatano ya Aprili 16, kwa uvamizi dhidi ya ofisi ya rais wa Burkina Faso, ambao ungefanywa na wanajeshi waliosajiliwa na maadui wa taifa.'' imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Waziri Sana.
Waziri wa ulinzi amesema waliopanga njama hizo dhidi ya nchi yake ni kundi la wapiganaji ambalo yeye anasema limeajiriwa na maadui wa nchi yake ambao hata hivyo hakuwataja, lakini akasema kundi hilo linapata hifadhi katika nchi jirani ya Ivory Coast.
Amesema kundi la wapiganaji hao linaundwa na wanajeshi wa zamani wa Burkina Faso na linaongozwa na Meja Joanny Compaore na Luteni Abdramane Barry.
Burkina Faso yainyooshea kidole Ivory Coast kuhusiana na njama hiyo
Burkina Faso imeilaumu nchi jirani ya Ivory Coast kwa kuwahifadhi wapinzani wake ambao siku zote wamekuwa wakipanga njama za kuipindua serikali ya kijeshi ya Kapteni Traore.
Hata hivyo, kufuatia jaribio hilo idadi kadhaa ya wanajeshi wakiwemo maafisa wawili wa vyeo vya juu walikamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio hilo la kuhatarisha usalama wa taifa.
Kwa takribani miaka miwili sasa utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso umekuwa ukiwahoji maafisa wengi wa kijeshi kwa tuhuma hizo hizo za kutaka kuzing'oa madarakani ngazi za utawala wa kisheria.
Traore amekuwa akitajwa kufanya mabadiliko kadhaa katika maeneo mbalimbali za kiuchuni na kijamii, lakini hali hii imezua mtafaruku na wahisani hasa nchi za Magharibi na Marekani.