Buriani Papa Yohanna Paulo II
3 Aprili 2005Kuchaguliwa kwake Karol WoJtyla kuwa Kiongozi w mku wa Kanisa Katoliki duniani kuliwashangaza wengi wakati ule.
Lilikua ni jambo ambalo hata wataliani hawakuweza kulifikiria kwamba Askofu mkuu huyo wa Krakau ndiye atakayekuwa Kiongozi mpya wa kanisa katoliki duniani Oktoba 16 1978, kwani hakuwa miongoni mwa walioangaliwa kuwa ni waliokua mstari wa mbele. Ilikua ni mara ya kwanza baada ya miaka 455 kuchaguliwa mtu asiye mtaliani kuliongoza Kanisa Katoliki.Mtangulizi wake Johanna Paulo wa kwanza alifariki siku 33 tu baada ya kushika wadhifa huo Sasa naye Papa Johanna Paulo wa pili ameiaga dunia Alikua Kiongozi wa Kanisa Katoliki aliyeliongoza kanisa hilo kwa muda mrefu zaidi.
Njia ndefu imefikia mwisho wake. Karol Wojtyla, alikua Baba mtakatifu ambaye vyombo vya habari daima vilikua daima na la kuripoti juu yake hadi mwisho wake. Alikua sio tu ni muakilishi wa jamii ya wakatoliki duniani, bali pia Kiongozi wa kidini aliye yazingatia kila siku masuala na matatizo mbali mbali ya ujumbe aliopewa. Ni Mwenyezi Mungu tu aliyeweza kulisimamisha jukumu lake hilo.
Kwa hakika hakuna Kiongozi wa kidini wala wa kisiasa wa karne iliopita na karne hii mpya aliyevuka mipaka ya kijografia na kuzizuru nchi nyingi katika mabara tafauti kama Yohanna Paulo wa pili. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani kutoka Poland alikua kichocheo kikubwa cha uadilifu katika enzi hii ya ustaarabu wa kisasa, dhidi ya maovu ya kila aina.
Karol Wojtyla alikua Papa wa kwanza ambaye daima alishughulikia pia masuala ya kisiasa. Alijiingiza kati panapohusika na mizozo, sio kwa silaha. Lakini silaha yake ulikua ni ujumbe-matamshi yaliokwenda mkono kwa mkono na diplomasia ya makao makuu ya Kanisa-Vatikani. Muongozo wake alioupa kipa umbele ulikua ni jukumu la kidini alilonalo, chini ya mtazamo wa mafundisho ya kristo. Alikutana na Viongozi mbali mbali na kuwaeleza alichofikiria. Kuanzia MiKhail Gorbachov na Fidel Castro, hadi Yassir Arafat na George Bush.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Yohanna Paulo wa pili, ina nafasi ya kipekee katika historia ya dunia. Kuchaguliwa kwake kama Baba Mtakatifu 1978, kulikua ni chachu ya mabadiliko katika kambi ya mashariki. Alisimama kidete dhidi ya ukandamizaji, ukosefu wa uhuru, ukiukaji wa haki za binaadamu na kupinga vikali vita- hadi dakika ya mwisho. Sambamba na hayo alitafuta kila nafasi ya kuleta maridhiano kati ya dini na tamaduni tafauti. Alikua Kiongozi wa kwanza kabisa wa Kanisa Katoliki kuzuru Msikiti na Sinagogi (Mahala pa ibada pa Wayahudi ).
Ujumbe wake mkubwa ulikua ni Amani. Mkutano wake mkuu pamoja na Viongozi wakuu wa dini nyengine kote duniani huko Assisi ni tukio la aina yake na hatua kubwa katika historia ya dini na ustaarabu.Kuona kwake mbali, kunatoa haja ya kupatikana mridhi wa aina yake wa wadhifa huo- kwa maneno ya mwandishi mmoja wa Kitalini-*Mkubwa kabisa miongoni mwa zile kubwa duniani.*