Bunge: Mpango wa kutokomeza umasikini Rwanda upitiwe upya
1 Aprili 2025Mwaka 2008 Serikali ilianzisha mpango wa kuwakwamua wananchi kutoka kwenye umaskini uliokithiri, hata hivyo wabunge wanasema, mpango huu umeshindwa kuleta mafanikio yaliyotegemewa. Kutoka Kigali, mwandishi wetu Sylivanus Karemera anaripoti zaidi.))
Kupitia mpango wa kupambana na umaskini, serikali ya Rwanda ilianzisha mkakati wa kuwasaidia wananchi maskini katika ngazi ya tarafa hasa wale ambao wanaishi maisha duni.
Ni mpango ulioanzishwa mwaka 2008 ambapo serikali inawapatia mikopo isiyo na riba wala masharti makubwa, mpango huu ulikwenda sambamba na kuwapa misaada ya pesa kidogo hasa wale wenye uwezo mdogo.
Hata hivyo wabunge wamesema kwamba miaka kumi na saba baadaye, mpango huu haujaleta matunda yaliyotarajiwa.
Soma pia:Oxfam: Utajiri wa mabilionea uliongezeka mno mwaka 2024
Wananchi wanasema masharti ya mpango huu ni mazito kiasi kwamba wengi wameamua kuachana nao na kubaki kwenye umaskini licha ya serikali kutangaza mara kwa mara kwamba inajitahidi kuwaondoa wananchi kutoka kwenye umasikini. Nyiransabimana Saidat na Ntibaziyandemye Bernard ni vijana wa mjini Kigali
"Kupata pesa siyo rahisi maana wanazingatia umri wa mtu, wakati sisi pia tunahitaji kupata pesa na bila wao kuyafanyia marekebisho masharti wasitegemee ikiwa suala la kupambana na umaskini miongoni mwa wananchi litawezekana, maana sisi pia tunahitaji kufanya kazi na miradi mbalimbali ya kujikimu, tunataka watupatie mitaji ambayo ni sawa na uwezo wetu"
Baadhi ya raia wanaonesha kuwa ni changamoto katika kufikiwa na mfumo wa fedha hizo, ambazo zinawalenga watu wenye kipato cha chini.
"Mtu akipata bahati na uwezo wa kupata pesa hizo, anaweza kubadili maisha yake kwa kufanya miradi midogomigodo lakini tatizo ni juu ya kuzipata pesa hizo au misaada mingine.Tunasikia kuna pesa na miradi ya kuwasaidia watu wenye uwezo mdogo kama sisi lakini hatuzipati, unajua miradi yoyote inakuwa na kianzio cha pesa lakini hatuna pesa hizo."
Malalamiko ya Wabunge juu ya mpango huo
Wabunge wameilalamikia serikali kwamba kila mwaka inatenga mabilioni ya pesa kuwasaidia wananchi wenye uwezo mdogo lakini kutokana na masharti magumu haziwasaidii wananchi hao na wala haziisaidii serikali kufikia mkakati wake wa kukabiliana na umaskini.
Uwamariya Odette na Mukandekezi Francoise ni wabunge katika bunge la Rwanda
"Haya masharti yanayowazuia watu walio na zaidi ya miaka 64 kuwa na haki katika misaada ya pesa hizo siyo mazuri, kwa sababu sisi tunajua kuwa mtu mwenye umri wa miaka 64 bado ni kijana kwakweli na wengi wanakuwa na elimu kiasi kwamba ukiwawezesha wanaweza kubuni miradi ya kujiendeleza." Alisema Uwamariya Odette mmoja wa Wabunge wanaotaka mpango huo ufanyiwe mapitio upya.
Soma pia:Wajerumani wengi ni masikini - Utafiti
Aliongeza kwamba "wananchi wengi walioko katika kundi hili wanaendelea kuuliza hatima yao na kusema kweli wana haki ya kuuliza hivyo maana kama nilivyosema hawa ni watu wenye akili na elimu na wenye uwezo wa kubuni miradi."
Kwa upande wake Mbunge Mukandekezi Francoise ambaye naye anaunga mkono mpango huo kufanyiwa marekebisho amesema kwamba "sharti jingine linasema kundi la watu hupewa mkopo endapo linaundwa na watu kuanzia miaka 18 lakini wasiozidi umri wa miaka 64, wananchi wanaendelea kulalamika kuwa mbona hata umri wa kuishi umeogenzeka nchini Rwanda kwa nini hilo pia msilizingatie na kutatua tatizo hili"
Serikali yakiri uwepo wa tatizo
Serikali imekiri kuwepo kwa tatizo lakini kwa maelezo ya waziri wa serikali za mitaa nchini Dr Patrice Mugenzi huenda sasa serikali ikalitathmini upya tatizo hilo.
"Tunaendelea kufanya mawasiliano na serikali kuona jinsi ya kutafuta uwezekano wa kuyaunganisha makundi haya katika mpango huu, tunatambua changamoto zilizopo na awali tulifikira kuwapa misaada ya moja kwa moja ya kiasi kidogo cha pesa lakini hilo tunaona halisaidii sana"
Soma pia:Robo ya watoto chini ya miaka 5 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula
Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema kwamba masharti lukuki hadi fedha hizo ziwafikie walengwa ni hatua ambayo haisaidii lolote katika mikakati ya kupambana na umaskini
Takwimu zinaonyesha kwamba hadi mwisho wa mwaka jana wa fedha pesa bilioni na milioni mbili faringa zilizokuwa zimelenga kuwasaidia makundi haya hazikutumiwa kutokana na mashariti hayo.