Bunge Ujerumani laridhia kupunguza wakimbizi
31 Januari 2025Mpango huo ulikubaliwa Jumatano jioni kwa msaada wa kura za chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD. Muswada uliopitishwa na bunge la Ujerumani Bundestag uliowasilishwa na kiongozi wa CDU Friedrich Merz anayetarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani unajumuisha kuwakataa waomba hifadhi wanaowasili katika mpaka wa Ujerumani, pamoja na kuwavua uraia watu wenye uraia pacha waliohukumiwa kwa makosa makubwa ya uhalifu.
Pendekezo hilo linalodhamiria kutaka sera kali zaidi za uhamiaji lilipitishwa kwa kura 348 dhidi ya 345, wakati wabunge 10 hawakupiga kura. Awali Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia kilisema kuwa kingeuunga mkono muswada huo.
Soma zaidi: Bunge la Ujerumani lajadili sera kali za uhamiaji
Muswada huo umepitishwa zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya uchaguzi wa mapema utakaofanyika Februari 23 huku AfD kinachofahamika kwa sera zake dhidi ya wahamiaji kikishika nafasi ya pili katika kura za maoni. Mpango huo uliopendekezwa na Merz, ulizua tafrani baada ya kiongozi huyo wa CDU kusema kuwa angekubali kuungwa mkono na AfD kama hilo lingehitajika ili kuupitisha.
Baada ya kupitishwa kwa muswada huo, mamia ya watu waliandamana mbele ya makao makuu ya chama cha CDU mjini Berlin wakipinga uamuzi huo.
Wakosoaji wapinga uamuzi wa bunge la Ujerumani
Msemaji wa masuala ya sheria aliyeshiriki katika maandamano Wiebke Judith ameelezea kusikitishwa kwake baada ya kupitishwa kwa muswada huo akisema, ''Hii ni ishara mbaya kwa wakimbizi. Kwa sababu pia inaonesha namna mambo yatakavyokwenda katika wiki na miezi ijayo kuelekea kuwekwa kwa vikwazo vikali zaidi dhidi ya wakimbizi. Na mgombea wa Ukansela wa CDU Friedrich Merz, ametangaza hasa kuwa anataka kufunga mipaka katika siku ya kwanza ya uongozi wake na atawarudisha wakimbizi mipakani bila hata ya kuuliza kilichowapata au wanakotokea. Hili litakuwa tatizo kubwa kwa watu wengi wanaotafuta kulindwa."
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema hatua ya muswada huo kupigiwa kura ya ndio ni dalili mbaya kwa taifa hilo. Kwa upande wake mgombea wa Ukansela kwa tiketi ya AfD Alice Weidel amesema kuwa kupitishwa kwa muswada huo ni jambo kubwa kwa demokrasia ya Ujerumani.
Ametoa wito pia kwa chama cha CDU kufikiria upya ikiwa bado kinataka kuendelea kuweka ukuta kati yake na AfD suala ambalo kwa maoni yake si la kidemokrasia. Kipindi cha nyuma, vyama vyote vikubwa vya Ujerumani vilisema kuwa visingeshirikiana na chama cha AfD.