Bunge lamuondolea kinga rais wa zamani wa Kongo
23 Mei 2025Hatua ya kuondolewa kinga kwa rais huyo wa zamani wa Kongo, kunafungua njia ya mashitaka dhidi yake kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, uhaini, na kushiriki katika harakati za uasi.
Kabila, ambaye aliiongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, anatuhumiwa na serikali ya Rais Félix Tshisekedi kushirikiana na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda, kundi ambalo limeteka maeneo makubwa ya mashariki mwa nchi hiyo. Rais Tshisekedi anadai kuwa Kabila alihusika katika kupanga njama na kundi hilo kupindua serikali yake kupitia mapinduzi.
Kabila aondolewa kinga ya kutoshitakiwa na Baraza la Seneti
Kiongozi huyo wa zamani hajakuwa nchini tangu mwaka 2023, na hakuhudhuria kikao cha Seneti kilichofanyika siku ya Alhamisi. Hadi sasa, haijulikani wapi alipo. Lakini Spika wa Seneti, Jean-Michel Sama Lukonde, alisoma uamuzi rasmi wa chombo hicho:
"Kwa hivyo, Seneti inaruhusu mashitaka na kuondolewa kwa kinga ya Joseph Kabila, seneta wa maisha," alisema Jean Lukonde.
Baada ya kuondoka madarakani, Kabila alipatiwa hadhi ya heshima kama seneta wa maisha – nafasi iliyompa kinga ya kibunge. Lakini sasa, kwa ombi la mwendesha mashitaka wa jeshi, kinga hiyo imeondolewa ili kuruhusu mchakato wa kisheria kuendelea. Kwa mujibu wa Seneta Carole Agito Amela, aliyewasilisha ripoti ya kamati maalum ya watu 40, kura zote ziliunga mkono hatua hiyo. Hata hivyo, wataalamu wa katiba wamehoji uhalali wa uamuzi huo, wakisema ulipaswa pia kupitishwa na Bunge la Kitaifa.
Msingi mkubwa wa kesi hiyo ni ushahidi uliotolewa na mwanasiasa wa upinzani Eric Nkuba, aliyedai kuwa alimsikia Kabila akimshauri kiongozi wa M23 kufanya mapinduzi dhidi ya Tshisekedi. Lakini mtafiti wa masuala ya siasa Ithiel Batumike amesema ushahidi huo ulitolewa kwa shinikizo.
Baadhi ya wanasiasa wasema hatua dhidi ya kabila ni ya kisiasa
Licha ya mashaka hayo, Seneti imeendelea na mchakato huo huku baadhi ya wanasiasa wakisema hatua hiyo ina sura ya kisiasa zaidi kuliko ya kisheria. Seneta Afani Idrissa Mangala anasisitiza umuhimu wa uchunguzi wa kina:
"Katika haki, ni lazima kufuatilia mambo hadi mwisho, na nadhani badala ya kufanya hisia tu, ni bora kuwa na uchunguzi wa kina zaidi na mashitaka yaliyojengwa kwa msingi imara zaidi, ambayo yataturuhusu kumweka mshitakiwa na upande wa mashtaka mezani," alisema Idrissa Mangala.
Kabila alikuwa ameashiria nia ya kurejea kwenye siasa na kutoa matamko ya kumkosoa Rais Tshisekedi. Tangu wakati huo, chama chake cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) kimezuwiwa na mali zake kadhaa kuvamiwa na maafisa wa usalama.
Serikali ya DRC yasimamisha shughuli zote za chama cha Kabila
Naibu Katibu Mkuu wa PPRD, Ferdinand Kambere, amesema mashitaka dhidi ya Kabila ni “usanii wa kisiasa” wa kuwapotosha raia kuhusu migogoro ya mashariki na rushwa. Wataalamu wa siasa, kama Christian Moleka, wanaonya kuwa hatua hiyo huenda ikachochea mgawanyiko zaidi wa kisiasa nchini humo.
Iwapo hatua hii itaonekana kama haki au njama ya kisiasa, bado haijulikani. Lakini ni wazi kuwa DRC imeingia katika awamu mpya ya mivutano ya kisiasa inayogusa moja kwa moja mustakabali wa usalama wa taifa.
afp/ap