Ulaya: Nchi za Afrika zinazominya wapinzani zinyimwe misaada
16 Julai 2025Hayo yameelezwa katika kikao cha Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya (DROI) kilichofanyika jana, ambapo Mbunge wa Bunge hilo, Michael Gahler, alikosoa vikali mwenendo wa kisiasa katika baadhi ya nchi za Afrika, akitoa mfano wa Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho kilichoshirikisha pia ujumbe wa Bunge la Afrika na Umoja wa Ulaya (OACPS), Gahler alitaka Umoja wa Ulaya usitishe misaada ya kifedha kwa nchi zinazominya uhuru wa vyama vya upinzani. Aidha, alisema haipaswi kutumwa waangalizi wa uchaguzi kwenye mataifa ambayo tayari matokeo yanajulikana kabla ya uchaguzi.
Gahler alitolea mfano kesi ya Tundu Lissu na kumkosoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Dk. Constantinos Kombos, aliyefanya ziara nchini Tanzania hivi karibuni, kwa kile alichokiita "kusifia hali ya kisiasa bila kuangalia hali halisi."
Gahler: Kesi ya uhaini inaichafua taswira ya Tanzania
Kauli hiyo ya Gahler imetolewa saa chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kusema mahakamani jana kuwa kesi yake ya uhaini inaichafua Tanzania mbele ya Jumuiya za Kimataifa.
Gahler pia aliwalaumu wawakilishi wa Umoja wa Ulaya waliopo barani Afrika kwa ukimya wao kuhusu hali ya kisiasa, na kuwataka wazungumze wazi kuhusu hali katika nchi wanazowakilisha.
Katika kesi hiyo ya uhaini iliyosikilizwa jana, Lissu aliyekuwa akijitetea mwenyewe, aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo haimhusu binafsi tu, bali inaiweka mahakama na taifa zima la Tanzania katika mtazamo wa Jumuiya za Kimataifa. Alisema kwa sasa anashikiliwa mahabusu pamoja na wafungwa waliopatikana na hatia ya kunyongwa.
Hoja hiyo ya athari za kimataifa imeungwa mkono na Dk. Richard Mbunda, Mhadhiri katika Shule ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wakati hayo yakiendelea, leo Tundu Lissu amepanda tena kizimbani kusikiliza uamuzi wa maombi ya marejeo, ambako anapinga hatua ya upande wa Jamhuri kutaka mashahidi watoe ushahidi wao kwa siri.
Mfululizo wa kesi hizi dhidi yake ulianza Aprili 10 aliposomewa kwa mara ya kwanza mashtaka ya uhaini na kutoa taarifa za uongo.