Bunge la Ujerumani lajadili ukomo wa deni la taifa
14 Machi 2025Bunge la Ujerumani linalokamilisha muda wake limefanya kikao maalumu kujadili kuifanyia mageuzi sheria ya ukomo wa deni la taifa, hatua ambayo yumkini ikairuhusu Ujerumani kutumia fedha nyingi katika masuala ya ulinzi na miundombinu.
Kansela mtarajiwa wa Ujerumani Friedrich Merz amesema hatua za haraka zinahitajika kuimarisha jeshi lenye raslimali chache na uchumi unaoyumba wakati alipokuwa akitetea mpango wa kuifanyia mageuzi sheria ya ukomo wa deni la taifa katika mjadala mkali bungeni uliofanyika hapo jana.
Muungano wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, pamoja na chama cha Social Democratic, SPD, vimekubaliana kuifanyia marekebisho sheria inayoweka ukomo wa deni la taifa ili kuruhusu matumizi makubwa zaidi katika ulinzi.
Akizungumza bungeni, kansela mtarajiwa Friedrich Merz alisema nyakati za kihistoria zinahitaji hatua za kihistoria. Merz amesema rais wa Marekani Donald Trump ameleta mabadiliko makubwa ulimwenguni na Ujerumani lazima ikope mabilioni ya fedha kufadhili ulinzi na miundombinu.
Aliongeza kusema Ujerumani lazima iwe tayari kujilinda yenyewe. Ujerumani inahitaji kurejea katika ulingo wa kimataifa kama mshirika wa kutegemewa barani Ulaya, katika jumuiya ya kijihami NATO na ulimwenguni kote.
Lars Klingbeil, kiongozi mwenza wa chama cha Social Democratic, SPD, amewatolea wito wabunge wajibu wito kwa hisotira akisema wana mpango unaoiunga mkono kwa kiwango kikubwa Ukraine, uwekezaji katika kuyalinda mazingira na ukuaji uchumi nchini Ujerumani.
Chama cha Kijani chamkosoa Merz, chataka mageuzi zaidi
Chama cha Kijani kinapinga mapendekezo ya mageuzi katika hali yake ya sasa, kikiwa na mtazamo tofauti. Kimeitisha mageuzi zaidi na uwekezaji zaidi huku kwa mara nyingine tena kikisema maamuzi yake ya kuyaridhia yatagemea mabadiliko hayo. Kimemtuhumu Merz kwa kutumia fursa kujinufaisha baada ya kukataa mapendekzo yao.
Kiongozi wa chama cha Kijani bungeni Katharina Dröge amemwambia kiongzi wa chama cha CDU Friedrich Merz kwamba kama anashangaa kwa nini mashauriano na wabunge wa chama cha Kijani yanakwenda jinsi yanavyokwenda, angemjibu na kumwambia ni kwa sababu hawategei neno lake.
Soma pia: Vyama vya Ujerumani vyafikiria kukopa zaidi
Ametaka kwamba azimio juu ya mpango maalumu wa fuko la miundombinu lijumuishe kipengee kinachosema uwekezaji utakaofadhiliwa na fedha hizo lazima uwe kweli wa nyongeza. Vinginevyo, Dröge alisema, kuna hatari kwamba fedha za mkopo zitaishia kutumika kwa ajili ya kupunguza kodi au miradi mingine.
Pili, Dröge ametaka kwamba upigaji kura kwa ajili ya matumizi ya ulinzi katika kuondolewa ukomo wa deni la taifa na fuko maalumu utenganishwe. Amehoji kwamba hakuna mahusiano yoyote kati ya mambo hayo mawili na bunge jipya la Bundestag lingeweza pia kupigia kura fuko maalumu la fedha katika tarehe ya baadaye.
Chama cha Kijani chatakiwa kiyaunge mkono mageuzi
Waziri Mkuu wa jimbo la kaszaini mashariki la Mecklenburg-Western Pomerania, Manuela Schwesig, wa chama cha SPD, amekitolea wito chama cha Kijani kiuunge mkono mpango huo wa fedha uliopendekezwa na muungano wa CDU/CSU na chama chake cha SPD. Amesema uchumi wa Ujerumani unahitaji uwekezaji, akiongeza kuwa suluhisho ni mageuzi ya sheria kuhusu ukomo wa deni la taifa.
Schwesig alisema ni wakati kwa vyama vya demokrasia vya Ujerumani kuziacha nyuma hisia za zamani na kuungana pamoja. Kwa mujibu wa Schwesig majimbo ya shirikisho la Ujerumani yanayaunga mkono mageuzi hayo.
Kwa upande wake mkuu wa chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD, Alice Weidel amesema chama chake kimewasilisha shauri katika mahakama ya katiba kulalamika kuhusu mpango huo wa mageuzi kikisema uamuzi unatakiwa kupitishwa na bunge lijalo linalotarajiwa kuapishwa mwisho wa mwezi huu.
Chama cha Die Linke chakosoa
Chama cha Die Linke kimeikosoa kura juu ya mpango huo kama hatua inayoiendea kinyume misingi ya demokrasia. Heidi Reichinnek, kiongozi mwenza wa chama cha kisoshalisti cha Die Linke, amesema kupigia kura mpango mpya wa fedha kutumia bunge linalokamilisha muda wake ni kinyume na demokrasia.
Vyama vya CDU/CSU na chama cha SPD vinataka kupitisha mageuzi ya kikatiba kulegeza ukomo wa deni la taifa kabla bunge jipya lililochaguliwa mwezi uliopita kuanza kufanya kazi Machi 25.
Kwa mujibu wa Reichinnek, chama cha SPD na muungano wa vyama vya CDU/CSU, vina wasiwasi kwamba huenda visipate theluthi mbili ya kura zinazohitajika katika bunge jipya, pia kutokana na kuongezeka kwa idadi ya viti bungeni vya chama cha Die Linke. Reichinnek amesema chama chake hakitauunga mkono mpango huo, ambao utaruhusu ongezeko la matumizi katika masuala ya ulinzi, akiutaja kuwa cheki ya wazi isiyo na kiwango maalum kwa kujihami na silaha.
Lindner: Mageuzi yataongeza mzigo kwa vizazi vijavyo
Kiongozi anayeondoka wa chama kilicho rafiki kwa wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP, Christian Lindner, ameukosoa mpango huo. Akizungumza bungeni, Lindner amesema mpango huo uliopendekezwa na vyama vya CDU/CSU na SPD utalegeza ukomo wa deni la taifa kiasi cha kusababisha kutowajibika na kufanya kazi ipasavyo na kusababisha mzigo mkubwa na shinikizo la kifedha kwa vizazi vya siku za usoni.
Lindner alisema mpango huu hauimarishi usalama wetu bali kinyume chake unachochea hatari mpya. Chama cha FDP hakitakuwa sehemu ya bunge lijalo baada ya kushindwa kufikisha kuvuka kiunzi cha asilimia 5 ya kura katika uchaguzi wa Februari.