Bundestag yapitisha mpango dhidi ya ukomo wa serikali kukopa
18 Machi 2025Mpango huo uliopitishwa na wabunge unalenga kulegeza sheria za katiba na kuondoa ukomo wa serikali kukopa na hivyo kufufua uchumi wa Ujerumani ambao ndio mkubwa zaidi barani Ulaya.
Ijumaa iliyopita, Friedrich Merz anayetarajiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani, alifikia makubaliano na chama cha Kijani juu ya mpango huo, huku Mahakama ya Katiba ya Ujerumani ikitupilia mbali pingamizi jipya la vyama vya upinzani dhidi ya mpango huo. Merz aliupigia upatu mpango huo akitaka upitishwe na bunge la sasa, akihofia kwamba huenda ukapingwa na bunge lijalo litakaloanza vikao vyake mnamo Machi 25.
Soma pia: Mahakama Ujerumani yausafishia njia mpango wa Merz wa ukopaji kujadiliwa bungeni
Mpango huo inajumuisha kuundwa kwa mfuko maalum wa euro bilioni 500 kwa ajili ya uwekezaji kwenye miundombinu katika muda wa miaka 12, lakini pia fedha za kufadhili mipango ya kuimarisha sekta ya ulinzi wa Ujerumani na hata Ulaya. Merz amesema kifurushi cha euro bilioni 3 kama msaada wa ziada kwa Ukraine kitatolewa kufikia Ijumaa hii.
Mpango huu ni wa kuwekeza zaidi kwenye ulinzi
Akizungumza mbele ya wabunge, Merz amesema kuna haja ya mpango huo kupitishwa haraka kutokana na kitisho cha Urusi akisema uvamizi wake nchini Ukraine ni vita dhidi ya Ulaya nzima, akitahadharisha kwamba Urusi yenye kupenda vurugu na Marekani isiyotabirika chini ya utawala wa Rais Donald Trump, ni mambo yanayoweza kulidhohofisha bara la Ulaya hadi kushindwa kujitetea.
"Uamuzi tunaochukua leo juu ya utayari wa nchi yetu kwenye suala la ulinzi unatafsirika kwa ujumla kama hatua kuu ya kwanza kuelekea jumuiya mpya ya ulinzi wa Ulaya, ambayo pia inazijumuisha nchi ambazo si wanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini ambazo zinadhamiria kujenga ulinzi huu wa pamoja wa Ulaya pamoja nasi, nazo ni nchi kama vile Uingereza na Norway."
Hata hivyo, CDU/CSU, SPD na chama cha Kijani vilihitaji kura 489 ili kutimiza theluthi mbili inayohitajika lakini hilo halikuwa tatizo kwa kuwa kwa pamoja walikuwa na kura 520 ambazo ni 31 zaidi ya zile zinazohitajika.
Mpango huu uliopitishwa katika Bunge la Shirikisho la Ujerumani, Bundestag, utatakiwa pia kupitishwa siku ya Ijumaa na Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani, Bundesrat. Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani, wanaupinga mpango huo wakisema utaitwika Ujerumani mzigo mkubwa wa madeni.
(Vyanzo: Mashirika)