Bunge la Ujerumani lajadili sera kali za uhamiaji
31 Januari 2025Muswada huo uliletwa bungeni na Kiongozi wa chama cha upinzani cha CDU Friedrich Merz aliyesema hatosita kushirikiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AFD kupitisha mapendekezo yake.
Katika hotuba yake kwenye bunge la Ujerumani Bundestag, ikiwa ni wiki moja baada ya shambulio la kisu katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Aschaffenburg, linalodaiwa kufanywa na raia wa Afghanistan, Kansela Olaf Scholz amesema haki ya kuomba hifadhi ni sehemu ya kanuni na mfumo halali wa sheria Ujerumani akisema kanuni zilizopo hazipaswi kutikiswa.
Scholz anayetafuta uungwaji mkono wa kurejea tena serikalini katika uchaguzi mkuu Ujao wa Februari 23 amesema mikakati iliyowekwa ambayo inajumuisha kuwakataa waomba hifadhi katika mipaka ya Ujerumani na kuwapokonya uraia wa ujerumani watu walio na uraia pacha waliohukumiwa kwa makosa ya uhalifu ni mambo yatakayoharibu utawala wa sheria na misingi ya Umoja wa Ulaya. Amesema Ujerumani ambayo ni nchi kubwa barani Ulaya itakuwa inavunja sheria ya Umoja huo.
Serikali ya Ujerumani, upinzani wakabiliana kuhusu sera za udhibiti wa mipaka
Licha ya hayo alitoa wito kwa Ujerumani kuanza utekelezwaji wa hatua ya kuwarudisha wahamiaji haramu makwao huku akisema watakaokubaliwa nchini ni wahamiaji halali ikiwa sheria zitatekelezwa kikamilifu.
Scholz amesema Ujerumani imeongeza takriban robo ya hatua za kuwaondoa wahamiaji haramu ukilinganisha na mwaka uliopita. Amesema Ujerumani inafuatilia kwa makini yanayoendelea nchini Syria na itaanza mara moja kuwarejesha nyumbani wahalifu kutoka nchi hiyo wakati hali itakaporuhusu ila kwa sasa amekiri kuwa ndege moja ya wahamiaji haramu iliondoka Ujerumani kwenda Afghanistan mwezi Agosti na nyengine inatarajiwa kuondoka hivi karibuni.
CDU yakosolewa kwa kuonesha nia kushirikiana na AFD
Wakati huo huo Kansela huyo wa Ujerumani amekosoa hatua ya chama cha CDU/CSU kuwa tayari kukubali kushirikiana na chama cha AfD kinachopinga wageni kusukuma mapendekezo yake juu ya uhamiaji na sera za mipakani akisema hilo ni jambo lisilosameheka.
"Wanakubali uugaji mkono wa chama cha AFD kwa mapendezo yao yaliyo kinyume cha sheria. Munawaunga mkono wale wanaopigana na demokrasia yetu, wanaochukia Umoja wetu wa Ulaya, wale wanaotia sumu nchini mwetu. hilo ni kosa kubwa lisilosameheka," alisema Sholz.
Uchaguzi wa Ujerumani: Kwanini Elon Musk anaipigia debe AfD?
Scholz ameonya kuwa muungano wa CDU/CSU unaweza kuungana na AfD baada ya uchaguzi wa Februari kuunda serikali licha ya Merz kukanusha mara kadhaa kwamba hilo haliwezi kutokea.
Katika mdahalo huo bungeni, kiongozi wa chama cha CDU fredirich Merz ametetea msimamo wake akisema demokrasia ya ujerumani ipo hatarini kutokana na wimbi kubwa la wahamiaji na sera za usalama. Amsema hakuna shaka kuwa demokrasia itakuwa hatarini iwapo chama cha mrengo wa kulia kitaingia madarakani lakini akatahadharisha pia kuwa demkrasia pia ipo hatarini wakati masuala muhimu kama ya kubana sheria za uhamiaji hazitotiliwa maanani.
Tayari chama kipya cha sera za mrengo wa kushoto cha Muungano wa Sahra Wagenknecht BSW kimesema wanachama wake watakataa mapendekezo ya CDU/CSU juu ya uhamiaji. Chama cha AFD kupitia naibu kiongozi wake Tino Chrupalla amesema chama hicho kitapigia kura mapendekezo hayo.
afp, ap, reuters