Kongo: Bunge lajadili mzozo wa mashariki mwa nchi
17 Machi 2025Akifungua kikao hicho cha Machi, spika wa Seneti Sama Lukonde aliwaomba Maseneta kuwa makini na hasa kuwa na nguvu ya kutosha, ili kukabiliana na changamoto zinazowasubiri katika kikao hiki.
"Tuaashirie kwamba kikao hiki kitamulika sana hali ya usalama inayojiri hapa nchini. Wakati tunafungua kikao hiki, miji mbalimbali, wilaya mbalimbali na vijiji mbalimbali vya mashariki mwa nchi yetu vinakaliwa na jeshi la Rwanda pamoja na vibaraka wa AFC-M23. Natilia hapa mkazo kwamba, ni wajibu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya juu chini, ili kupata suluhu kwa tatizo hilo."
Kikao cha Machi kinafunguliwa wakati ambapo miji muhimu, ikiwa ni pamoja na Goma na Bukavu, pamoja na vijiji kadhaa, imeshatekwa na waasi wa AFC-M23.
Wabunge na Maseneta wanakabiliwa na jukumu zito, kwani wakaazi wa maeneo haya wanawategemea wao kwa suluhisho la kudumu.
Soma pia:M23: Serikali ya DRC inahujumu mazungumzo ya Angola
Aidha, kikao hiki kinafunguliwa huku serikali ya Kongo ikiwa imekubali kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja na waasi.
Uamuzi huu umeibua hisia tofauti miongoni mwa raia wa Congo, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Félix Antoine Tshisekedi alikuwa akishikilia msimamo wake wa kutokuketi meza moja na waasi. Hata hivyo, baada ya ziara yake mjini Luanda, mazungumzo ya moja kwa moja yametangazwa rasmi.
Ikumbukwe kuwa, swala la vita mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilikuwa likipuuzwa na wabunge wengi, huku baadhi wakidai kuwa vita hivyo vinawahusu tu watu wa eneo hilo.
Hata hivyo, hali ya sasa inaonyesha mabadiliko, huku wabunge na maseneta wa maeneo mengine ya Congo wakionyesha mshikamano dhidi ya tatizo hili.
Rais Tshisekedi aisaka amani ya Kongo nje ya Afrika
Wakati huo huo, Rais Félix Tshisekedi amekutana na mbunge wa Marekani, Ronny Jackson, kujadili hali ya usalama mashariki mwa Congo pamoja na fursa za uwekezaji wa Marekani nchini humo.
Serikali ya Kongo bado haijafafanua mpango wowote wa ushirikiano wa madini kwa usalama, ingawa inasisitiza kutafuta washirika mbalimbali wa kimataifa.
Jackson, ambaye ametajwa kama mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa Marekani inataka kuona Congo ikiwa katika hali ya utulivu ili kuvutia wawekezaji wa sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na kobalti, lithiamu, na urani.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kitaifa Vital Kamerhe, katika ufunguzi wa kikao cha bunge, alitangaza furaha yake kuhusu vikwazo vilivyochukuliwa na mataifa mbalimbali, ikiwemo Ujerumani, dhidi ya Rwanda.
Soma pia:Jumuiya ya SADC yaamua kuondoa vikosi vyake mashariki mwa DRC
Alitumia fursa hiyo kumuweka Rais Félix Antoine Tshisekedi kwenye mikono ya Mwenyezi Mungu, ili amuongoze katika mchakato wa kutafuta amani ya kudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hata hivyo, waasi wa M23 wametuhumu serikali ya Kongo kwa kujaribu kuvuruga mazungumzo ya amani kwa kutumia ndege za kivita na droni kushambulia maeneo yenye raia. Hali hii imeibua mashaka kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani.
Mazungumzo ya moja kwa moja baina ya wajumbe wa serikali ya Kongo na waasi wa AFC-M23 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Machi 18 mjini Luanda.