Bunge la Kenya lamtaka Ruto atoe ushahidi wa madai ya rushwa
22 Agosti 2025Spika Moses Wetang'ula, Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung'wah na Kiongozi wa Wachache Junet Mohammed, wamesema madai kwamba wabunge hupokea hongo lazima yawekwe wazi kwa ushahidi kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa.
Akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Uongozi wa Bunge la Kitaifa unaoendelea jijini Mombasa, Spika Moses Wetang'ula alisema wabunge wanapaswa kujitahidi kurejesha imani ya wananchi kwa Bunge. Hata hivyo, aliongeza kuwa matamshi ya Rais yanaidhalilisha asasi hiyo. "Kwa maoni yangu, matamshi hayo yanasalia madai. Lakini lazima tutafakari nafsi zetu kwa uzito. Pia kama taifa, bila uadilifu, uongozi hauna maana — unafeli.” alisema Wetang'ula.
Maseneta na Wabunge wazidi kumshinikiza
Wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa pamoja kati ya wabunge wa UDA na ODM Ikulu, Nairobi, Rais Ruto aliibua shutuma hizo lakini hakuwataja kwa majina wabunge anaowatuhumu kwa kuomba hongo ili kupitisha miswada fulani.
Maseneta na wabunge sasa wanamshinikiza Rais Ruto kufichua majina ya wabunge wanaodaiwa kupokea hongo na vyanzo vya madai hayo. Kwa upande wake, Bunge linamtuhumu Rais kwa kulichafulia jina bila ushahidi. Ruto, akirejelea mjadala wa hivi karibuni kuhusu Sheria ya Mgongano wa Maslahi, alisema mbunge mmoja alidai shilingi milioni kumi kama hongo ili kupitisha mswada.
Kiongozi wa Wachache Bungeni, Junet Mohammed, alisema: "Mtu anayekuja na madai hayo lazima athibitishe. Mzigo wa ushahidi uko kwa yule anayetoa madai hayo; alete ushahidi.”
Haya yanajiri huku Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ikisema haina ushahidi wowote unaowaunganisha wabunge na madai hayo, lakini imeahidi kuanzisha uchunguzi na kuunga mkono kikosi kazi cha mashirika mbalimbali cha kupambana na ufisadi.