Bunge la Israel lapitisha sheria tata ya mageuzi ya mahakama
27 Machi 2025Sheria hiyo iliidhinishwa kwa kura 67 dhidi ya moja iliyopinga huku upande wa upinzani ukisusia kikao hicho cha asubuhi.
Kwa ujumla, bunge hilo lina wabunge 120. Kura hiyo inaakisi azma ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu ya kuendelea na mpango wake wenye utata wa mageuzi ya mahakama, ambao uliibua mojawapo ya vuguvugu kubwa zaidi la maandamano katika historia ya Israel mnamo mwaka 2023 kabla ya kuzuka kwa vita vya Gaza.
Dakika chache baada ya kura hiyo, Yair Lapid, kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, alitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba amekata rufaa katika mahakama ya juu dhidi ya sheria hiyo kwa niaba ya vyama kadhaa vya upinzani.
Kulingana na waziri wa haki Yariv Levin, aliyewasilisha muswada wa sheria hiyo, hatua hiyo ililenga kudumisha usawa kati ya nguzo za serikali za bunge na mahakama.