Bundesliga kuanza kutimua vumbi Agosti 22
26 Juni 2025Kulingana na Bodi ya Ligi ya Soka ya Ujerumani (DFL) mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu itafanyika kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Munich Ijumaa, Agosti 22.
DFL imewataka mashabiki siku ya Alhamisi kuingia kwenye app ya Bundesliga ili kujua michezo mingine itakayochezwa kwenye ufunguzi. Lakini watalazimika kushiriki michezo ya mafumbo ama "puzzles" ili kujua michezo hiyo.
DFL hata hivyo itachapisha ratiba nzima ya Ligi ya Bundesliga siku ya Ijumaa, Juni 27, 2025.
Cologne yaahidi "makubwa" baada ya kurejea Bundesliga
Mambo yanazidi kuhanikiza wakati klabu zikijiandaa kuanza msimu mpya. Kocha mpya wa Klabu ya Cologne Lukas Kwasniok ameahidi makubwa baada ya klabu hiyo kurejea kwenye ligi kuu ya Bundesliga.
Cologne "The Billygoats" walijikuta wakimalizia msimu uliopita bila ya kocha licha ya kupanda daraja, baada ya mazungumzo na kocha wa muda Friedhelm Funkel kutozaa matunda.
"Mimi ni mwalimu mwenye hisia na hapa ni mahali pa hisia kwa hivyo tunashabihiana," alisema kijana huyo mwenye umri wa miaka 44 alipozungumza kwenye mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari kuhusiana na kibarua chake kipya siku ya Jumatano.
"Kama mnataka mtu asiyekuwa na mvuto, nadhani mimi sio mtu sahihi." Kwasniok alikuwa akiifundisha timu ya Paderborn iliyopo kwenye daraja la pili, na taarifa za awali zilisema huenda angeenda kuifundisha Hoffenheim.
"Hatimaye nimetimiza ndoto yangu ya kuifundisha timu inayoshiriki ligi ya Bundesliga"