BRUSSELS:Jitahada zimeanza kuachiliwa kwa shehena ya nguo kutoka China.
30 Agosti 2005Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya-UE,Peter Mandelson,ameanza jitahada kuhakikisha shehena ya mamilioni ya nguo kutoka China zinazoshikiliwa na maofisa wa forodha wa Umoja huo zinaachiliwa.
Bwana Mandelson ameeleza matumaini yake kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya watakubaliana kulipatia muafaka suala hilo hivi karibuni.
Kamishna huyo amekwishaanza mazungumzo na nchi moja moja wanachama wa EU,kabla hajawasilisha mapendekezo yake yatakayosaidia kumaliza mzozo huo baadae wiki hii.
Nchi za Uholanzi,Denmark,Sweden,Finland na Ujerumani, zimeonya kuwepo uwezekano wa watu kukosa ajira miongoni mwa wafanyabiashara wa rejareja,iwapo Umoja wa Ulaya hautoregeza msimamo wake kwa bidhaa kutoka China zinazoingia katika nchi za Umoja huo.
Lakini nchi ambazo pia hutengeneza nguo kama Ufaransa,Italia na Uhispania zimedhamiria kuendelea na msimamo wao waliouanza tangu mwezi wa Juni juu ya bidhaa zinazoagizwa nje.