BRUSSELS : Wasi wasi barani Ulaya juu ya homa ya mafua ya ndege
14 Oktoba 2005Umoja wa Ulaya unachukuwa hatua kali kuzuwiya kuenea homa ya mafua ya ndege ambayo imefika kwenye mipaka ya Ulaya.
Waatalamu wa maradhi ya wanyama wa Umoja wa Ulaya leo wanatazamiwa kuidhinisha hatua za tahadhari za ziada baada ya kirusi cha ugonjwa huo kuthibitishwa kuwepo nchini Uturuki. Umoja wa Ulaya umezitaka serikali za umoja huo kuchukuwa hatua haraka za kulimbikiza madawa ya kupambana na ugonjwa huo wa mafua ya ndege.
Umoja wa Ulaya umepiga marufuku uingizaji wa ndege walio hai kutoka Uturuki na Romania ambapo maafisa wa afya wamegunduwa virusi vya ugonjwa huo kwa bata.Udhibiti mkali pia umewekwa kwenye viwanja vya ndege na mipakani.Umoja wa Ulaya pia unapendekeza kutowa tahadhari za safari na kupiga marufuku kuwinda.
Shirika la Afya Duniani WHO limewataka watu wasihofu na kusema kwamba kimsingi homa ya mafua ya ndege ni ugonjwa wa wanyama.