BRUSSELS : Viongozi wa Ulaya wakutana kuimarisha uchumi
22 Machi 2005Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo hii kwa mkutano wao wa siku mbili wa majira chipukizi wenye lengo la kufunguwa nafasi zaidi za ajira na kufufuwa uchumi unaozorota wa bara hilo.
Mkutano huo utalenga katika kuianzisha upya Agenda ya Lisbon mradi wa kifahari uliozinduliwa mwaka 2000 kwa lengo la kuifanya Ulaya kuwa na uchumi utakaotowa ushindani mkubwa kabisa ifikapo mwaka 2010.
Hata hivyo Benki ya Dunia imeonya kwamba mabadiliko ya kuregeza kanuni za bajeti za Umoja wa Ulaya yanaweza kudhoofisha sarafu ya euro.Mawaziri wa fedha wa Ulaya hapo Jumapili walikubaliana kupunguza makali ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya wa kukuza uchumi na uthabiti wa sarafu ya euro kwa kuziruhusu serikali kuongeza madeni na kukiuka kikomo cha nakisi ya bajeti cha asilimia tatu kwa kuzingatia masharti fulani.
Muongozo tata unaokusudia kuwepo kwa ridhaa zaidi katika sekta ya kutowa huduma ya Ulaya pia utajadiliwa.