Brussels. Marekani yaomba rasmi msaada.
4 Septemba 2005Umoja wa Ulaya na shirika la kujihami la mataifa ya magharibi NATO , wamesema leo kuwa wamepokea ombi rasmi kutoka Marekani kwa msaada wa dharura katika majimbo yaliyoathirika na kimbunga Katrina.
Umoja wa Ulaya umesema kuwa Marekani imeomba msaada wa vifaa vya huduma ya kwanza , mablanketi, magari ya kubebea maji, pamoja na makasha 500,000 ya vyakula vilivyokwisha tayarishwa.
Kamishna wa Umoja huo Stavros Dimas amesema katika taarifa kuwa umoja wa Ulaya uko tayari kuchangia katika juhudi zenye lengo la kupunguza hali mbaya ya kimaisha inayokutikana katika mji wa New Orleans.
Nato imesema kuwa Marekani imeomba msaada wa chakula kutoka shirika hilo.
Nchini Italia ndege ya kijeshi iliyobeba shehena ya vitu mbali mbali vinavyohitajika kwa wahanga wa kimbunga Katrina nchini Marekani inatarajiwa kuondoka leo Jumapili usiku kwenda nchini Marekani.
Ndege hiyo imebeba , mablanketi, makoti, shuka za kutandika katika vitanda , maboti ya plastiki yanayojazwa upepo, vifaa vya kusafisha maji pamoja na vifaa vya huduma ya kwanza vitu ambavyo vitagawiwa kwa watu wapatao 15,000.
Msemaji wa idara ya ulinzi wa raia nchini Itali Luca Spoletini amesema ndege hiyo itaondoka leo usiku baada ya kutua katika miji kadha nchini humo ikikusanya vifaa hivyo.
Rais Bashar al – Assad wa Syria ameeleza masikitiko makubwa ya nchi yake kwa wahanga wa maafa yaliyosababishwa na kimbunga Katrina.
Amesema kuwa wakati akitoa rambirambi zake kwa niaba ya wananchi wa nchi hiyo , pia amesikitishwa sana na maafa yaliyowapata wahanga na familia zao.
Ameongeza kuwa ana imani kubwa kuwa Wamarekani wana uwezo mkubwa wa kupambana na maafa hayo pamoja na matokeo yake.
Wakati huo huo watu walionusurika na kimbunga Katrina wameanza kuondolewa kwa safari za ndege kwenda katika maeneo salama katika kile kinachoelezwa kuwa ni uhamishwaji mkubwa kabisa kuwahi kutokea katika historia ya Marekani.
Maafisa wanaofanyakazi ya uokozi wamesema kuwa kiasi cha watu 40,000 wameondolewa katika maeneo yaliyoathirika na kimbunga Katrina katika mji wa New Orleans.