BRUSSELS Benita Ferrero Waldner kukutana na viongozi wa Ukraine.
17 Februari 2005Kamishna wa umoja wa Ulaya anayehusika na uhusiano wa mataifa ya kigeni, Benita Ferrero-Waldner, atakwenda Ukraine kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo, siku chache kabla umoja huo kuidhinisha mpango utakaounganisha uhusiano wake na taifa hilo la Urusi ya zamani. Halmashauri ya umoja wa Ulaya imetangaza itakutana na rais wa Ukraine, Viktor Yuschenko, pamoja na waziri mkuu, Yulia Tymoschenko na maafisa wa baraza lake la mawaziri mjini Kiev. Mpango wa Brussels unapendekeza faida kumi kwa Ukraine, zikiwemo faida za kibiashara na utoaji wa visa za kusafiria, lakini hautaji ikiwa umoja huo utaliunga mkono pendekezo la Ukraine kutaka kujiunga na jumuiya ya Ulaya. Wakati huo huo, mawaziri wa fedha wa umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kujadili mpango wa kudumisha uchumi, utakaoziwekea viwango vya bajeti nchi wanachama. Ujerumani imelalamika kwamba mpango huo ni kikwazo kikubwa cha uchumi.