BRICS wakutana chini ya kivuli cha vita vya ushuru vya Trump
6 Julai 2025Mataifa 11 yanayoinukia kiuchumi — yakiwemo Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini — yanawakilisha takriban nusu ya idadi ya watu duniani na asilimia 40 ya pato la uchumi wa dunia.
Jumuiya hiyo, ijulikanayo kama BRICS, imegawanyika kuhusu masuala mengi, lakini imeungana katika msimamo dhidi ya tawala wa Rais wa Marekani na vita vyake vya ushuru vinavyokatizwa na kuanzishwa kila mara.
BRICS inatarajiwa kueleza "wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hatua za ushuru na zisizo za ushuru za upande mmoja," ikionya kuwa hatua hizo ni haramu na za kiholela, kwa mujibu wa rasimu ya taarifa ya mkutano ambayo shirika la habari la AFP limepata nakala yake.
Mwezi Aprili, Trump alitishia washirika na mahasimu kwa ushuru mzito, lakini baadaye alisitisha kwa muda kufuatia kuyumba kwa masoko ya fedha.
Trump na Waziri wake wa Fedha, Scott Bessent, walionya kuwa watarejesha ushuru wa upande mmoja kwa washirika wao endapo hawatakamilisha makubaliano hadi Agosti Mosi.
BRICS yaikosoa Marekani bila kumtaja Trump moja kwa moja
BRICS itatoa onyo kuwa hatua kama hizo zinakiuka kanuni za biashara za dunia, "zinatishia kupunguza zaidi biashara ya kimataifa” na "zinaathiri matarajio ya ukuaji wa uchumi duniani.”
Rasimu ya tamko la mkutano huo haiitaji Marekani wala rais wake kwa jina, lakini ni wazi kuwa ni kejeli ya kisiasa inayoelekezwa kwa Rais wa Marekani.
Taasisi ya masuala ya uchumi ya kimataifa ya Peterson, yenye makao yake mjini Washington inakadiria kuwa ushuru wa Trump unaweza kupunguza ukuaji wa Pato la Taifa la Marekani kwa asilimia mbili na kuathiri uchumi wa mataifa mbalimbali kutoka Mexico hadi eneo lenye mafuta la Ghuba ya Kiarabu.
BRICS, iliyobuniwa miaka 20 iliyopita kama jukwaa la mataifa yanayokua kwa kasi, sasa inaonekana kama chombo kinachoongozwa na China ili kupinga ushawishi wa mataifa ya Magharibi.
Lakini kutokana na kupanuka kwake na kujumuisha mataiafa kama Iran, Indonesia na mengine, jumuiya hiyo imekuwa na changamoto ya kufikia msimamo wa pamoja kuhusu masuala kama vita vya Gaza na mabadiliko ya taasisi za kimataifa.
Kutokuwepo kwa viongozi wakuu kwapunguza mvuto wa mkutano
Mkutano wa mwaka huu umepoteza mvuto wake wa kisiasa kutokana na kutokuwepo kwa Rais wa China Xi Jinping, ambaye kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 12 hatohudhuria.
Rais huyo wa China siyo pekee aliyeamua kutokuwepo. Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita, naye hakuhudhuria binafsi, lakini alishiriki kwa njia ya video.
Katika hotuba yake, aliwaambia viongozi wenzake kuwa ushawishi wa BRICS "unaendelea kukua” na kuongeza kuwa jumuiya hiyo imekuwa mdau muhimu katika uongozi wa dunia.
Hata hivyo, kutokuwepo kwa Xi ni pigo kwa BRICS na kwa Rais mwenyeji Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil, ambaye anataka nchi yake iwe na nafasi kubwa zaidi kimataifa.
Jumapili, aliwapokea viongozi katika Ghuba ya kuvutia ya Guanabara mjini Rio, na kuwaambia kuwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa uko chini ya mashambulizi, huku akiikosoa NATO na Israel.
Lula aikosoa NATO na Israel, asema amani inapuuzwa
Aliilaumu jumuiya ya ulinzi ya NATO kwa kuchochea mashindano ya silaha kwa kuhimiza wanachama wake kutumia asilimia 5 ya Pato la Taifa katika ulinzi.
"Ni rahisi zaidi kuwekeza kwenye vita kuliko kwenye amani,” alisema, huku akiishutumu Israel kwa kuendesha "mauaji ya halaiki” katika Ukanda wa Gaza.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, ambaye nchi yake bado inakabiliana na athari za mzozo wa siku 12 na Israel, pia hakuhudhuria mkutano, lakini aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi.
Chanzo kimoja cha karibu na mazungumzo ya mkutano kilisema kuwa Iran ilitaka karipio kali zaidi dhidi ya Israel na Marekani kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vituo vya kijeshi, nyuklia na vingine nchini Iran.
Hata hivyo, afisa mmoja wa kidiplomasia alisema rasimu ya tamko hilo itatoa "ujumbe uleule” ambao BRICS ilitoa mwezi uliopita.
BRICS yatoa wasiwasi mkubwa, lakini yaepuka kutaja wahusika moja kwa moja
Wakati huo, washirika wa Tehran walieleza "wasiwasi mkubwa” kuhusu mashambulizi dhidi ya Iran, lakini hawakuitaja wazi Israel wala Marekani.
Hali hii inaashiria changamoto ya kufikia muafaka mkali miongoni mwa wanachama wa BRICS, licha ya kuunganishwa na matarajio ya kupinga upande mmoja wa utawala wa Marekani.
Licha ya upanuzi wake na ongezeko la umuhimu wake wa kimataifa, BRICS bado inasitasita kuchukua msimamo wa moja kwa moja dhidi ya mataifa yenye nguvu, kutokana na tofauti za kimaslahi na kiitikadi kati ya wanachama wake.
Lakini kwa ujumla, tamko hilo linaonesha nia ya BRICS kuwa sauti mbadala ya ushawishi wa Magharibi na kutafuta mfumo mpya wa uongozi wa dunia unaojumuisha mataifa yote kwa usawa.
Katika mazingira haya ya mvutano wa kibiashara na kisiasa, BRICS inaendelea kujijenga kama jukwaa linaloweza kuunganisha mataifa yanayoinukia kwa malengo ya pamoja ya maendeleo na ushawishi wa kidiplomasia.