Bodi ya Bayern yaridhia uwezekano wa kumsajili Tah
13 Mei 2025Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich wanaripotiwa kukaribia kumsajili beki wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani Jonathan Tah kwa uhamisho huru. Tah anaihama klabu ya washindi wa Bundesliga mwaka 2024 Bayer Leverkusen baada ya miaka 10 itakapofika mwiho wa msimu.
Gazeti la Bild limeripoti Jumanne kwamba bodi ya usimamizi ya Bayern iliidhinisha uwezekano wa uhamisho wa Tah siku moja kabla.
Ripoti hiyo inasema Bayern wanaahidi kumpa beki wa kati Tah mwenye umri wa miaka 29 mkataba wa miaka mitatu hadi 2028. Bodi ya usimamizi ya Bayern lazima ikubaliane kuhusu mikataba yote mikubwa ya uhamisho na usajili wa wachezaji.
Tah tayari alihusihwa na kuhamia klabu ya Bayern mwaka uliopita, lakini viongozi wa Levekusen na Bayern hawakuweza kuafikiana kuhusu kitita cha fedha za uhamisho.
Tah alisema siku ya Jumapili baada ya mechi ya mwisho nyumbani BayArena na klabu yake ya Leverkusen kwamba angetangaza kuhusu mustakhbali wake katika wiki chache zijazo. Amependekeza hangesita kukubali uhamisho nje ya nchi na amewahi kuhusishwa na vinara wa ligi ya La Liga nchini Uhispania, Barcelona, lakini haijabainika wazi kama wana uwezo kifedha kumsajili.