Bochum yatangazwa mshindi mgogoro wa mechi na Union
28 Aprili 2025Mgogoro ambao umekuwa ukiendelea kwa kipindi kirefu umefika mwisho Jumatatu wakati klabu ya Bochum iliporuhusiwa kubaki na ushindi iliyoupewa baada ya kipa wake kupigwa na kifaa cha kuwashia moto kutoka kwa viti vya mashabiki. Ushindi wa Bochum katika mzozo huo huenda usitoshe kuiokoa kutokana na shoka la kushuka daraja.
Hukumu ya mahakama ya soka ya Ujerumani ilikataa rufaa kutoka kwa klabu ya Union Berllin zaidi ya miezi minne tangu mechi yake dhidi ya Bochum ilipokamilika katika mazingira ya kutatanisha.
Timu hizo mbili zilikuwa zinaelekea kutoka sare 1-1 mjini Berlin mnamo Desemba 14 wakati kipa wa Bochum Patrick Drewes alipopigwa kichwani. Pambano hilo lilisimamishwa na Drewes akapewa matibabu. Waamuzi wa mchezo huo waliamua kuendelea na mechi nusu saa baadaye bila Drewes, ambaye aligoma kuendelea kucheza. Kocha wa Bochum alisema timu yake ilikuwa inacheza chini ya mazingira ya kugoma.
Timu hizo mbili zilikubaliana kucheza dakika chache zilizosalia bila kushambulia na kipyenga cha mwisho kilipulizwa zikiwa sare 1-1 huku wachezaji wakisimama na kufanya mazungumzo.
Mwezi mmoja baadaye, mahakama ya michezo ya shirikisho la soka la Ujerumani iliipa Bochum ushindi wa goli 2-0, ikihoji kwamba Union ilikuwa na dhamana kwa shabiki wake kumjeruhiwa kipa Drewes na kuifanya timu ya Bochum kudhoofika.
Union Berlin ilikata rufaa
Rufaa zilifuata katika miezi ya hivi karibuni kutoka kwa klabu ya Union Berlin, ambayo ilionya juu ya kuwepo na njama chafu na vilabu vingine vikawa na wasiwasi huenda vikapoteza ikiwa Bochum itapanda juu kwenye jedwali.
Akitangaza hukumu ya Jumatatu, mwenyekiti wa mahakama Udo Steiner alisema kulikuwa na mazingira ya mechi kutelekezwa kabla kukamilika wakati timu hizo mbili zilipokubaliana kutokufungana. Kwa hiyo ni halali kisheria kuamua matokeo hayo kwa ajili ya Bochum kana kwamba mechi hiyo haikuendelea kabisa. Hukumu hiyo ilithibitisha maamuzi mara mbili yaliyotolewa awali yaliyoipendelea Bochum.
Mchakato wa kisheria uliendelea kwa muda mrefu vya kutosha kwa Union na Bochum kucheza tena katika mechi ya marudiano Jumapili na kutoka sare 1-1.
Kupata alama mbili kwa ushindi badala ya sare, kunayaimarisha matumaini hafifu ya Bochum kuepuka kushuka daraja. Bochum ikipoteza mechi yake dhidi ya Heidenheim Ijumaa itakuwa na maana kwamba kwa hakika wanashuka katika daraja la pili msimu ujao, ikiwa ni baada ya miaka minne kucheza katika ligi kuu.